• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Inter Milan wakataa Eriksen awachezee baada ya kupata matatizo ya moyo wakati wa fainali za Euro 2020

Inter Milan wakataa Eriksen awachezee baada ya kupata matatizo ya moyo wakati wa fainali za Euro 2020

Na MASHIRIKA

CHRISTIAN Eriksen hajakubaliwa kusakata soka nchini Italia msimu huu baada ya kupata matatizo ya moyo akichezea Denmark kwenye fainali zilizopita za Euro 2020 dhidi ya Finland.

Haya ni kwa mujibu wa klabu ya Inter Milan ambayo imemwajiri Eriksen katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29 alianguka na kuzima ghafla wakati wa kipute dhidi ya Finland mnamo Juni 2021.

Japo Eriksen aliwekewa kifaa cha kudhibiti mapigo ya moyo almaarufu ICD, Inter wameshikilia kwamba hawatamruhusu kuwachezea na watakuwa radhi kumwachilia mwishoni mwa msimu huu ili atafute hifadhi kwingineko.

Hata hivyo, haijulikani iwapo vikosi vya mataifa mengine vitamkubalia Eriksen kuendelea kutandaza soka ikizingatiwa kwamba ana kifaa cha ICD.

Beki wa zamani wa Manchester United anayechezea Ajax, Daley Blind aliwahi pia kuwekewa ICD baada ya kupatikana na tatizo la misuli ya moyo. Licha ya hali hiyo, sogora huyo raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 31 aliendelea kusakata boli katika Ligi Kuu ya Eredivisie na timu ya taifa ya Uholanzi.

Eriksen aliwajibikia Tottenham Hotspur kwa misimu sita na nusu na alikuwa sehemu ya kikosi kilichozidiwa ujanja na Liverpool kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019. Aliingia katika sajili rasmi ya Inter Milan kwa ada ya Sh2.6 bilioni mnamo Januari 2020.

You can share this post!

Liverpool kualika Leicester huku West Ham wakiendea Spurs...

Monterrey washinda taji la tano la Concacaf na kufuzu kwa...

T L