• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 10:55 AM
Jamhuri ya Czech na Croatia waambulia sare kwenye gozi la Euro

Jamhuri ya Czech na Croatia waambulia sare kwenye gozi la Euro

Na MASHIRIKA

JAMHURI ya Czech ilijiweka pua na mdomo kufuzu kwa hatua ya 16-bora kwenye fainali zinazoendelea za Euro baada ya kuwalazimishia Croatia sare ya 1-1 mnamo Juni 18, 2021 uwanjani Hampden Park.

Jamhuri ya Czech waliwekwa kifua mbele katika dakika ya 37 kupitia penalti iliyochanjwa na fowadi Patrik Schick. Refa Carlos del Cerro alilazimika kurejelea teknolojia ya VAR kubainisha kwamba beki Dejan Lovren alikuwa amemchezea Schick visivyo kabla ya kuwapa Jamhuri ya Czech penalti hiyo.

Lovren aliyekosa mechi ya ufunguzi iliyokutanisha Croatia na Uingereza mnamo Juni 13, alimpiga Schick kumbo puani wakati wakiwania mpira wa hewani.

Schick ambaye ni fowadi wa Bayer Leverkusen katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), alimwacha hoi kipa Dominik Livakovic na kuwa mwanasoka wa kwanza kuwahi kufunga mabao matatu kutokana na mechi mbili za kwanza za Euro tangu Mario Mandzukic wa Croatia afanye hivyo mnamo 2012.

Bao la Jamhuri ya Czech liliwazindua Croatia waliokita kambi langoni mwa wapinzani wao ila wakashindwa kufunga goli huku Ante Rebic akipoteza nafasi kadhaa za wazi.

Hata hivyo, masogora hao wa kocha Zlatko Dalic walilazimika kusubiri hadi dakika ya 47 kabla ya kusawazishiwa na Ivan Perisic aliyeshirikiana vilivyo na Andrej Kramaric.

Perisic ambaye ni fowadi wa Inter Milan, ndiye mwanasoka wa kwanza wa Croatia kuwahi kufunga bao katika mashindano manne tofauti ya haiba kubwa kimataifa yakiwemo Kombe la Dunia mnamo 2014, Euro 2016, Kombe la Dunia 2018 na Euro 2020.

Mechi kati ya Jamhuri ya Czech na Croatia ilikuwa ya pili kuwahi kukutanisha vikosi hivyo tangu viambulie sare ya 2-2 kwenye hatua ya makundi ya Euro mnamo 2016 nchini Ufaransa.

Ni kwa mara ya kwanza tangu fainali za Kombe la Dunia za 2006 kwa Croatia kutosajili ushindi kwenye mechi mbili za ufunguzi wa mapambano ya haiba kubwa kimataifa.

Ingawa Jamhuri ya Czech hawajawahi kushinda Croatia katika majaribio manne ya awali, masogora hao wa kocha Jaroslav Silhavy wanadhibiti kilele cha Kundi D kwa alama nne sawa na Uingereza ambao wana mabao machache. Croatia wanakamata nafasi ya tatu kwa alama moja sawa na Scotland walio na mabao machache.

Croatia wameratibiwa kuvaana na Scotland katika mechi ya mwisho ya Kundi D mnamo Juni 22 huku Jamhuri ya Czech wakipimana ubabe na Uingereza ya kocha Gareth Southgate.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kiungo Christian Eriksen wa Denmark arejea nyumbani baada...

Wakenya matumaini tele mashindano ya kutafuta tiketi ya...