• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Kiungo Christian Eriksen wa Denmark arejea nyumbani baada ya kuondoka hospitalini

Kiungo Christian Eriksen wa Denmark arejea nyumbani baada ya kuondoka hospitalini

Na MASHIRIKA

KIUNGO matata wa Inter Milan na timu ya taifa ya Denmark, Christian Eriksen, ameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji ulioshuhudia akiwekewa kifaa maalum cha kuwezesha moyo kuanza kufanya kazi mara moja iwapo atakabiliwa tena na mshutuko wa moyo (ICD).

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 alipata matatizo ya moyo mnamo Juni 12 katika uwanja wa Parken jijini Copenhagen wakati akiwajibikia Denmark dhidi ya Finland kwenye fainali za Euro.

Baada ya kuondoka hospitalini, Eriksen alizuru kikosi cha Denmark kambini kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani akiandamana na familia yake.

“Asanteni sana kwa wingi wa salamu. Imekuwa tija na fahari tele kuona na kuhisi ukubwa wa kiwango cha msaada wenu. Upasuaji ulifanyika vyema na naendelea kupata nafuu,” ikasema sehemu ya taarifa ya Eriksen kwa kusisitiza kwamba atakuwa mstari wa mbele kushangilia Denmark dhidi ya Urusi katika mchuano wa mwisho wa Kundi C mnamo Juni 20.

Eriksen ambaye ni kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspur, alianguka ghafla uwanjani na kuzimia mwishoni mwa kipindi cha kwanza dhidi ya Finland. Alipelekwa hospitalini baada ya maafisa wa afya kuhakikisha kwamba amepata fahamu.

Tukio hilo lilifanya gozi kati ya Denmark na Finland kusitishwa kwa zaidi ya saa mbili kabla ya kurejelewa na Finland wakasajili ushindi wa 1-0.

Denmark walitandaza mchuano wao wa pili katika Kundi B mnamo Juni 17 jijini Copenhagen na wakapokezwa na Ubelgiji kichapo cha 2-1. Mechi hiyo iliwapa mashabiki, maafisa wa mechi na mashabiki fursa ya kumstahi Eriksen, kusimama naye na kumtakia nafuu ya haraka.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uswidi wapepeta Slovakia na kujiweka pazuri kuingia hatua...

Jamhuri ya Czech na Croatia waambulia sare kwenye gozi la...