• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kane atoa pumzi Ujerumani, Italia ikimumunya Hungary

Kane atoa pumzi Ujerumani, Italia ikimumunya Hungary

NA MASHIRIKA

MUNICH, UJERUMANI

KOCHA Gareth Southgate ameridhika na kikosi chake baada ya kutoka sare ya 1-1 na wenyeji Ujerumani, katika pambano la Ligi ya Mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League) ugani Allianz Arena jijini Munich mnamo Jumanne.

Nahodha Harry Kane aliifungia Uingereza bao la kusawazisha kupitia mkwaju wa penalti, na kuhitimisha mabao 50 ambayo amefunga kimataifa.

Penalti hiyo ilipeanwa na teknolojia ya VAR baada ya Kane kuangushwa katika kijisanduku hatari na Nico Schlotterbeck.

Ujerumani walimiliki na kutawala mechi kwa kiasi kikubwa, lakini masogora wa kocha Hansi Flick walikosa kutumia vyema nafasi nyingi kujiweka pazuri.

Kiungo mshambuliaji Kai Havertz alivurumisha kombora kali lililomsumbua kipa Jordan Pickford, kabla ya beki Kyle Walker kuvuruga juhudi za Thomas Muller dakika chache baadaye.

Mashambulizi yao, hata hivyo, yalizaa matunda shuti la Jonas Hofmann lilipotumbukia wavuni dakika ya 50.

Uingereza walikuwa wakikodolea macho kichapo cha pili baada ya kufinywa 1-0 na Hungary siku ya Jumamosi.

Kane alianza kuchanganya ngome ya Ujerumani mechi ikielekea kumalizika, juhudi zake zikivurugwa na Manuel Neuer aliyeokoa mipira kadhaa hatari kiwemo kona iliyokuwa ikielekea langoni.

Mshambuliaji huyo matata wa Tottenham alikosa kufunga tena alipobakia pekee na kipa Neuer.

Baada ya mechi kocha Flick alikiri hawakuzoa matunda kamili kwa mchezo wao mzuri.

“Tulistahili kufunga bao la pili. Hata hivyo, tulionyesha kiwango chetu kizuri uwanjani,” akasema Mjerumani huyo.

Naye kiungo Ilkay Gundogan alihoji: “Tulilemea wapinzani vipindi vyote ila walibahatika kuwasazisha zikibakia dakika chache mechi iishe.”

Kane alikuwa mwingi wa furaha kutinga goli hilo.

“Nimefurahi, ingawa nilikuwa na nafasi nyingi za kutinga magoli zaidi. Tulicheza dhidi ya wapinzani wakali lakini tulionyesha uwezo wetu,” akaongeza.

Beki Kieran Trippier alimpongeza nahodha wake kwa bao hilo muhimu.

Akaongeza: “Matokeo ya leo ni ya kujivunia. Tutakutana kuchambua makosa ili tucheze vizuri zaidi mechi ijayo.”

  • Tags

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Tufanye nini kwenye hafla ya...

Mwalimu Mkuu aliyekaidi korti aepuka jela kwa kulipa faini...

T L