• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
KCB FC yakung’uta Bidco, Eastlanders kirafiki Ligi Kuu ikinukia

KCB FC yakung’uta Bidco, Eastlanders kirafiki Ligi Kuu ikinukia

Na GEOFFREY ANENE

WANABENKI wa KCB FC wameendelea kuandikisha matokeo mazuri wakijiandaa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu 2022-2023 baada ya kupepeta Bidco United 2-1 ugani Thika katika kaunti ya Kiambu mnamo Agosti 25.

Wanamafuta wa Bidco walitangulia kutetemesha nyavu za KCB dakika ya 10. Hata hivyo, vijana wa kocha Zedekiah ‘Zico’ Otieno walisawazisha 1-1 kabla ya mapumziko kupitia kwa Edmond Edema naye Francis Kahiro akapachika bao la ushindi dakika 20 baadaye.

Ushindi huo ulipatikana siku moja baada ya KCB kunyamazisha Eastlanders FC 3-1 uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi mnamo Agosti 24.

Henry Ochieng’ alipatia KCB uongozi mapema katika kipindi cha kwanza kabla ya Allan Ogedo na Kennedy Owino kuongeza mabao mawili katika dakika za lala-salama.

Otieno alisema kuwa amefurahishwa na vijana wake. “Tumetathmini kiwango cha usawa wa kimwili wa timu kabla ya msimu wa Ligi Kuu ya 2022-2023. Wanaonekana kuwa tayari kushindana na wako katika hali nzuri,” alisema Otieno.

Hata hivyo, Otieno alieleza kusikitishwa na uamuzi wa Mahakama ya Kusikiliza kesi za michezo (SDT) kufutilia mbali matokeo ya msimu 2021-2022.

“Inahuzunisha kuwa watu wanaofanya maamuzi haya si wadau katika soka. Makocha, wachezaji na marefa hawajazungumza. Kama taifa tunastahili kuchukulia soka yetu kwa uzito na kusuluhisha masuala haya,” alisema.

Mshambulizi wa zamani wa Gor Mahia FC, Nicholas Kipkurui, ambaye amejiunga na KCB kwa kandarasi ya mwaka mmoja, hakushiriki mechi dhidi ya Eastlanders.

KCB pia imekamilisha kusaini mabeki Maurice Ajwang’ na Kevin Otieno kujaza nafasi za Robinson Kamura na Baraka Badi waliohama. Mfungaji bora wa ligi msimu ulipita Derrick Otanga pia amehama KCB na kujiunga na CS Constantine nchini Algeria. Msimu mpya utaanza Septemba 10.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona, Bayern Munich na Inter Milan watiwa katika kundi...

Man-City wapewa Chelsea, Arsenal wakionana na Brighton...

T L