• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kenya Police kuanzisha timu ya kandanda ya wanawake

Kenya Police kuanzisha timu ya kandanda ya wanawake

NA RUTH AREGE

TIMU ya Kenya Police FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la nchini (FKF-PL), iko mbioni kuanzisha timu ya wanawake.

Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu hiyo Chris Oguso M’mbwanga amesema baada ya kusimamia ufufuaji Police FC kutoka daraja la Supa Ligi (NSL) anaamini kuwa wakati umefika wa kukuza soka ya wanawake.

“Ndoto ya kuwa na timu ya Wanawake yangalipo hai, tukikumbuka kuwa ni hitaji la Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Zaidi ya hayo, kama huduma, tuna wanaume na wanawake ambao uwakilishi wao unapaswa kutambuliwa kwa kuwa na timu ya wanawake,” Oguso aliongeza.

“Natumai, msimu ujao tutakuwa na timu iliyoundwa. Kinachoturudisha nyuma kwa sasa ni bajeti kwa kuwa tunategemea wafadhili wetu Betika, huduma za ndege za Air 748 na marafiki,” Oguso aliongezea.

Afisa huyo wa Polisi aidha alisema, klabu hiyo sasa inatafuta washirika zaidi ambao watasukuma fedha zaidi kusaidia kuanzisha timu za wanawake na vijana.

“Pia tutatoa ombi la unyenyekevu kwa Inspekta Jenerali wetu wa Polisi na Naibu wake, kuruhusu wanawake ambao watakuwa wanachama wa timu waliosajiliwa katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi. Hili litawatia moyo wachezaji pakubwa na wakati huo huo kupunguza suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa wachezaji wetu,” aliongezea Oguso.

Police FC kwa sasa, wako katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa FKF-PL na alama 49 kutokana na mechi 27, alama 13 nyuma ya vinara Gor Mahia walio na alama 62.

Ulinzi Stars ndio timu pekee inayoshiriki ligi kuu ya wanaume na timu ya wanawake, Ulinzi Starlets. Katika Ligi Kuu ya Kitaifa (NSL), Vihiga United na Vihiga Queens zinamilikiwa na Serikali ya Kaunti ya Vihiga, huku Kaunti ya Kisumu ikiunga mkono Kisumu All Stars na Kisumu All Starlets ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL).

Miezi miwili iliyopita, Police FC ilizindua uwanja wao wa Kenya Police Sacco katika mtaa wa Nairobi South B ambao uko chini ya Hazina ya Police Sacco.

  • Tags

You can share this post!

Wang’ara na teknolojia ya kutafsiri lugha kurahisisha...

Mafuriko yaua watu 130 nchini Rwanda

T L