• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kenya Prisons yazoa medali tano siku ya kwanza ya judo

Kenya Prisons yazoa medali tano siku ya kwanza ya judo

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imezoa medali tatu za fedha na mbili za shaba katika siku ya kwanza ya mashindano ya judo ya vikosi vya usalama ya Afrika Mashariki mjini Moshi, Tanzania hii leo.

Katika uzani wa chini ya kilo 52, Decy Amolo (Kenya Prisons) aliridhika na nishani ya fedha baada ya kupoteza dhidi ya Uwiwana Julienne kutoka Burundi Police katika fainali. Amolo alikuwa amemlea Hezakimana Nada (Burundi Police) katika nusu-fainali.

Katika uzani wa kilo zisizozidi 57, Becky Jebet (Kenya Prisons) alipoteza dhidi ya Irakiza Ines (Burundi Police) katika fainali. Jebet alikuwa amezidia maarifa Latifa Abdalla Kambi (Tanzania Defence Forces) katika nusu-fainali. Monica Mumbi (Kenya Prisons) ameambulia medali ya fedha ya uzani wa chini ya kilo 48 baada ya kupata kisiki katika  fainali dhidi ya Kanyamuneza Signoline (Burundi Police).

Kitengo hiki kilivutia washiriki wawili pekee. Walioshindia Kenya medali za shaba ni John Nderitu na Brian Obwogo kutoka Kenya Prisons. Nderitu alimzidi nguvu Oscaris Richard (Magereza Tanzania) katika mchuano wa kuamua nambari tatu katika uzani wa kilo zisizozidi 66. Alikuwa amepoteza dhidi ya Thomas Mwenda (Magereza Tanzania) katika nusu-fainali.

Katika uzani wa kilo chini ya 73, Obwogo aliridhika na shaba baada ya kumlemea Aron Phillipo (Tanzania Defence Forces). Obwogo alikuwa amepoteza dhidi ya Philemoni Kaberege (Magereza Tanzania) katika nusu-fainali. Jumamosi itakuwa zamu ya Peterson Gathiru, Samson Wambi, Robinson Samora na Kimani George na kinadada Shagillah Odacho, Diana Kana, Emmah Gatwiri, Lydia Barongo, Caroline Odongo, Millicent Matende na Joyce Chepchumba. Aidha, kikosi cha Polisi cha Kenya kilithibitisha Ijumaa kuwa hakitashiriki makala hayo ya kwanza ya judo yaliyovutia timu kutoka Tanzania, Zanzibar, Burundi na Kenya Prisons.

Malkia mpya wa Afrika Perister ‘Nyasuu’ Bosire na mwanaolimpiki Levy Sang ni baadhi ya wachezaji matata wa Kenya Police waliotarajiwa kutetemesha katika mashindano hayo.

You can share this post!

Shirikisho la Hoki Afrika latangaza washiriki wa Kombe la...

Leads kutetea taji la Tim Wanyonyi dhidi ya wazoefu

T L