• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kenya yateremka kwenye jedwali la FIFA la viwango vya ubora

Kenya yateremka kwenye jedwali la FIFA la viwango vya ubora

NA JOHN ASHIHUNDU

KICHAPO cha majuzi dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya kimataifa kimeathiri pakubwa timu ya Harambee Stars kulingana na orodha ya viwango iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Alhamisi.

Kulingana na orodha hiyo, timu hiyo ya kocha Engin Firat imeshuka nafasi nne kutoka 105 hadi 109.

Licha ya mwito wa Rais William Ruto kuomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu hiyo wakati wa mechi hiyo ya kirafiki, Stars ilichapwa 1-0 na Sudan Kusini inayoorodheshwa katika nafasi ya 167 katika viwango hivyo.

Tito Okello anayechezea klabu ya Kenya Police alifunga bao hilo, hii ikiwa historia kwa taifa hilo kushinda Kenya.

Okello alifunga bao hilo baada ya kumchanganya mlinzi Joseph Onyango anayesakata soka nchini Ufaransa.

Stara ilipoteza mechi hiyo baada ya washambuliaji Michael Olunga na Masoud Juma kupoteza nafasi nyingi katika mechi hiyo.

Wakenya walitarajia Stars kushinda mechi hiyo, siku chache tu bada ya kuandikisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Qatar mjini Doha.

Mbali na kushindwa na Sudan Kusini, kufuzu kwa Tanzania kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kunamweka kocha Firat katika hali ngumu kutokana na presha ya mashabiki, wakati huu kikosi chake kinajiandaa kushiriki mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2026. Mchujo huo unaanza Novemba, 2023.

Akijitetea, Firat amesema hakuna mikakati ya kuiwezesha timu hiyo kuvuma katika mechi za kimataifa, huku akiongeza kwamba hajalipwa kwa miezi kadhaa, madai ambayo yamesababisha mvutano mkubwa kati ya FKF na Serikali.

Harambee Stars imepangiwa katika kundi moja na Ushelisheli, Burundi, Gambia na Ivory Coast, ambapo timu itakayomaliza katika nafasi ya kwanza itafuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa kwa pamoja na Amerika, Canada na Mexico.

Uganda inayoorodheswa katika nafasi ya 89 dunaini inaendelea kuongoza msimamo wa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, licha ya kutofuzu kwa fainali za 2024 AFCON zitakazofanyika nchini Côte d’Ivoire.

Morocco inaongoza orodha ya mataifa ya Afrika kwenye viwango hivyo vya kimataifa ikishikilia nafasi ya 13, mbele ya Senegal (20), Tunisia 29, Algeria (34) na Misri (35).

Mabingwa wa Dunia, Argentina wanaendelea kuongoza kimataifa wakifuatwa na Ufaransa, Brazil, Uingereza na Ubelgiji katika Tano Bora.

  • Tags

You can share this post!

MTANIKUMBUKA: ‘Utabiri’ wa Uhuru umetimia?

Madiwani 28 watia saini kuidhinisha mchakato wa kumbandua...

T L