• Nairobi
 • Last Updated April 17th, 2024 5:55 AM
Kiatu cha Dhahabu: Wendy Atieno na Airin Madalina wahemeshana

Kiatu cha Dhahabu: Wendy Atieno na Airin Madalina wahemeshana

NA AREGE RUTH

WASHAMBULIZI Airin Madalina (Bunyore Starlets) na Wendy Atieno (Thika Queens), wanahemeshana katika kuwania kiatu cha dhahabu Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) wakiwa na mabao 17.

Imesalia mechi moja msimu wa 2022/23 kutia kikomo lakini, haitabiriki ni nani atakuwa mfungaji bora msimu huu hadi mechi ya mwisho itakapochezwa wikendi.

Kati ya mabao 17 ambayo Madalina na Atieno wamefunga, wamefunga penalti moja na tatu mtawalia.

Atieno angefunga mabao mengi zaidi msimu huu lakini, alipata jeraha la pua na mdomo baada ya kugongana na kipa wa Zetech Sparks Sherly Chaviha wakati wa mechi ya KWPL mnamo Machi 5, 2023 katika uwanja wa Cambridge katika Kaunti ya Kajiado. Thika ilipoteza mechi hiyo 1-0.

Kwa sasa anavalia barakoa spesheli ya usoni kwa kimombo ‘Facial Nose Guard’.

Kwa upande mwingine, hata ingawa Airin anaongoza kwenye chati ya wafungaji bora, timu yake iko katika hatari ya kushuka daraja. Wikendi hii wanakibarua dhidi ya Nakuru City Queens na lazima wapate ushindi kukwepa shoka la kushuka daraja.

Washambulizi wengine; Puren Alukwe (Zetech Sparks), Monicah Etot (Kisumu All Starlets) na Elizabeth Muteshi (Nakuru City Queens) wanafunga tano bora na mabao 15, 13 na 12 mtawalia.

Mara ya mwisho Alukwe kucheka na wavu, alifunga bao moja katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Kisumu katika uwanja Ruaraka jijini Nairobi Alhamisi iliyopita.

“Puren amekuwa wa msaada mkubwa kwetu msimu huu. Kufunga kwake mabao kulitutoa kwenye eneo la kushushwa daraja,” alisema kocha wa Zetech Bernard Kitolo baaada ya mechi yao dhidi ya Kisumu Alhamisi iliyopita.

Katika timu ya Gaspo Women, ushindani mkali ulishuhudiwa kutoka kwa Lydia Akoth na Wambui Mutukiza ambao wana mabao 12 na 11 mtawalia.

Msimu jana, mshambulizi wa zamani wa mabingwa watetezi Vihiga Queens Topister Situma alituzwa kiatu cha dhahabu baada ya kufunga mabao 17. Huenda mabao mengi zaidi yatapachikwa msimu huu.

Wafungaji bora.

 1. Airin Madalina (Bunyore Starlets FC) – 17
 2. Wendy Atieno (Thika Queens FC)-  17
 3. Puren Alukwe (Zetech Sparks FC) -15
 4. Monica Etot (Kisumu All Starlets FC) -13
 5. Elizabeth Muteshi (Nakuru City Queens FC) -12
 6. Jackline Chesang’ (Wadadia Women FC) -12
 7. Lydia Akoth (Gaspo Women FC) -12
 8. Maureen Achieng (Vihiga Queens FC) -12
 9. Mutukiza Wambui (Gaspo Women FC) -11
 10. Anitah Namatah (Vihiga Queens FC) -10
 • Tags

You can share this post!

Madereva 34 waingia WRC Safari Rally tayari kuonyeshana...

Ruto amteua mke wa Chebukati awe mwenyekiti wa CRA

T L