• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
Waiguru na Wangui Ngirici wazika tofauti zao

Waiguru na Wangui Ngirici wazika tofauti zao

NA MWANGI MUIRURI

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru kwa mara ya kwanza amekumbatiana hadharani na kusalimiana na aliyekuwa mpinzani wake Wangui Ngirici katika mji wa Kagio walipokuwa wanamsubiri Rais William Ruto anayefanya ziara katika eneo la Mlima Kenya.

Wapinzani hao wamesalimiana na kukumbatiana kwa furaha huku pia wakitenga muda wa kupigwa picha ya pamoja.

Dkt Ruto wakati wa ziara hiyo, amewaambia wakazi wa mji wa Kagio kwamba serikali ya Kenya Kwanza inajitolea kikamilifu kuhakikisha tatizo la ajira linashughulikiwa.

Amesema wanaopinga Sheria ya Fedha ya 2023 ni maadui wa maendeleo.

Ushuru wa Ujenzi wa Nyumba za Gharama nafuu, Dkt Ruto amesema, unalenga kusaidia kubuni nafasi za ajira kwa vijana.

Aidha, amewahimiza vijana kutumia ujuzi wao kujitafutia riziki mitandaoni, akisema ujenzi na uzinduzi wa vituo vya masuala ya kidijitali unaendelea katika maeneo mbalimbali kote nchini.

Rais William Ruto akizindua mradi wa Sh1.2 bilioni wa usambazaji maji wa Kerugoya-Kutus katika mji wa Kagio, Kaunti ya Kirinyaga mnamo Agosti 5, 2023. PICHA | JOSEPH KANYI

Kiongozi wa nchi pia amesisimua wakazi kwa kusema haoni haja ya kuagiza vitanda kutoka mataifa ya kigeni kama China.

“Wapende wasipende hawataagiza vitanda kutoka China na Marekani. Mwenye hataki kulalia kitanda ambacho kimetengenezwa na hawa vijana alale chini. Kwani ndipo usingizi upatikane ni lazima kitanda kiwe kimetoka China?” ameuliza Rais Ruto.

Kiongozi wa nchi anafanya ziara ya siku tano katika eneo hilo la Mlima Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Azimio kuwapa wafuasi mwelekeo Septemba

Kibera Girls na Soccer Assassins vitani kutafuta mshindi wa...

T L