• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Kibiwott Kandie na Peres Jepchirchir waendea mataji ya New York Marathon

Kibiwott Kandie na Peres Jepchirchir waendea mataji ya New York Marathon

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia mbio za wanaume za kilomita 21, Kibiwott Kandie atashiriki mbio zake za kwanza kabisa za kilomita 42 wakati wa makala ya 50 ya New York Marathon nchini Amerika mnamo Novemba 7.

Mwanajeshi huyo anajivunia kukamilisha mbio za kilomita 21 kwa dakika 57:32 kutokana na ushindi wake wa taji la Valencia Half Marathon nchini Uhispania mnamo Desemba 6, 2020.

Muda huo ni rekodi ya Kenya, Afrika na Dunia mbio za kilomita 21.

Jijini New York, Kandie atakutana na bingwa wa Berlin Marathon mwaka 2016 na 2019 Kenenisa Bekele, Mholanzi mwenye asili ya Somali Abdi Nageeye aliyenyakua nishani ya fedha kwenye Olimpiki za Tokyo 2020, Mkenya Albert Korir, Muethiopia Girma Bekele Gebre, bingwa wa dunia 2015 na mshindi wa New York Marathon 2016 Ghirmay Ghebreslassie (Eritrea) na Waamerika Jared Ward na Ben True.

Kenenisa Bekele amevizia rekodi ya dunia ya saa 2:01:39 inayoshikiliwa na Mkenya Eliud Kipchoge mara kadhaa na huenda hii ni fursa nyingine na pengine yake ya mwisho kujaribu kuifuta.

Bekele anayejivunia mataji mengi ya dunia mbio za nyika, Riadha za Dunia na Olimpiki, alikosa rekodi ya Kipchoge kwa sekunde mbili jijini Berlin mwaka 2019 alipotwaa taji kwa saa 2:01:41.

Kitengo cha kinadada pia kimevutia majina makubwa akiwemo Mkenya Peres Jepchirchir, ambaye ni bingwa wa Olimpiki, Molly Seidel aliyeridhika na medali ya shaba kwenye Olimpiki mjini Sapporo nchini Japan, mshindi wa nishani ya fedha ya marathon kwenye Riadha za Dunia 2019 na bingwa wa Tokyo Marathon 2019 Ruti Aga.

Waamerika Aliphine Tuliamuk na Sally Kipyego, ambao walizaliwa Kenya, pia watashiriki, ingawa bingwa wa Boston Marathon 2018 Des Linden amejiondoa.

Muethiopia Ababel Yeshaneh na Mkenya Nancy Kiprop pia watatifua vumbi jijini New York pamoja na dada ya mwanaolimpiki Bernard Lagat, Viola Lagat, atatimka marathon kwa mara ya kwanza kabisa.

You can share this post!

CHEPKWONY: Wanafunzi wapewe fursa ya kujieleza, washauriwe

Maskini jeuri wakataa chakula kwa sababu ya siasa

T L