• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Maskini jeuri wakataa chakula kwa sababu ya siasa

Maskini jeuri wakataa chakula kwa sababu ya siasa

Na MAUREEN ONGALA

WAKAZI wa eneobunge la Ganze, Kaunti ya Kilifi, walisusia chakula cha msaada walichopelekewa na Gavana Amason Kingi kutokana na mizozo ya kisiasa.

Ubishani ulikuwa umeibuka kati ya wafuasi wa Bw Kingi wanaounga mkono chama anachohusishwa nacho cha Pamoja African Alliance (PAA) na wale wa ODM katika hafla ya uzinduzi wa barabara.

Hafla hiyo ya kuzindua barabara ya Bamba-Ganze-Kilifi iliongozwa na Waziri James Macharia, na ilikuwa imetangulia usambazaji wa chakula cha msaada kutoka kwa serikali ya kaunti.

Eneo hilo ni mojawapo ya yale ambayo yamekumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji kutokana na athari ya kiangazi cha muda mrefu.

Bw Macharia, Kamishna wa Kaunti ya Kilifi, Bw Kutswa Olaka, na wageni wengine ambao si wanasiasa waliondoka mara moja kutoka hafla hiyo dalili za mifarakano ya kisiasa zilipoanza kuonekana.

Ni wakati wa utumbuizaji ambapo kiongozi wa vijana anayeegemea upande wa Bw Kingi alielekea jukwaani na kuanza kumiminia sifa PAA, hatua iliyoghadhabisha wafuasi wa ODM.

Wafuasi hao wa ODM walisikika wakisema “Ganze hatupai”.

Mabishano yaliendelea kwa karibu dakika 15, na Bw Kingi alipoenda jukwaani, alizomewa na umati uliokataa kumsikiliza.

“Nimewaletea chakula, na yeyote anayetaka anifuate hadi katika afisi ya Kaunti Ndogo ya Ganze,” akawaambia.

Hata hivyo, wakazi walikataa wito huo.

“Ilikuwa ni makosa Bw Kingi kuanza hotuba yake kwa kuambia wananchi amewafaa kwa kuwaletea chakula cha msaada. Tulitarajia aliposimama angetuliza watu, lakini akawakejeli kwa njaa yao kisha akaondoka na kikosi chake,” akasema Bw Fikirini Jacobs ambaye ni kiongozi wa kikundi cha vijana Ganze.

Wanachama wa ODM, wakiongozwa na Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo, walimkashifu gavana kwa kutaka kugeuza hafla muhimu kuwa ya kupigia debe chama chake cha PAA.

Mbunge wa Ganze ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM Kilifi, Bw Teddy Mwambire, alisema alitarajia gavana kuzungumzia masuala muhimu katika hafla hiyo wala si kuigeuza kuwa ya kisiasa.

You can share this post!

Kibiwott Kandie na Peres Jepchirchir waendea mataji ya New...

TAHARIRI: Serikali ilijikwaa kwa kutangaza likizo fupi

T L