• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
CHEPKWONY: Wanafunzi wapewe fursa ya kujieleza, washauriwe

CHEPKWONY: Wanafunzi wapewe fursa ya kujieleza, washauriwe

Na KIPKOECH CHEPKWONY

VISA vya wanafunzi kugoma na kuteketeza mabweni vinazua taharuki kubwa kote nchini.

Visa hivi vimesababisha uharibifu wa mali yenye thamani ya mamilioni ya pesa.

Angalau shule 10 zimeripoti kutokea kwa visa vya uchomaji wa mabweni tangu taasisi za masomo zifunguliwe Januari.

Mkasa wa juzi ni ule wa shule ya upili ya wasichana ya Buruburu ambayo imefungwa kwa muda usiojulikana huku tayari wanafunzi 59 wakilazwa hospitalini. Ni changamoto inayotatiza masomo haswa kabla ya mitihani ya kitaifa inayotarajiwa kufanywa Machi 2022.

Maswali halisi ya kujiuliza ni pamoja na: Ni nini chanzo cha moto katika shule za Kenya? Nani wa kulaumiwa au kuwajibika visa vya moto vinavyotokea? Ni hatua gani ya kuchukuliwa ili kukabiliana na tatizo hili?

Malalamiko yanayotajwa mara nyingi miongoni mwa wanafunzi ni pamoja na wakuu wa shule kuwa na mamlaka kupita kiwango, lishe duni ya shule na rasilimali duni za kujifunzia. Nyingi za shutuma hizi zinaonyesha tuhuma kuhusu jinsi bajeti za shule zinavyogawanywa.

Wakuu wa shule za sekondari wanasema kuwa kipindi cha wiki 11 kwa kuwa cha masomo chini ya tarehe za muhula zilizorekebishwa kimeweka shinikizo kwa watoto kuonyesha tabia za ‘kupotoka’.

Katika baadhi ya matukio, wanafunzi wanalaumu usimamizi wa shule kwa kushindwa kusikiliza matakwa yao.

Mnamo 2018 wanafunzi wa shule moja ya wavulana waliteketeza shule kwa kunyimwa fursa ya kutazama mechi ya Kombe la Dunia.

Wanafunzi wakinyanyaswa shuleni haswa za sekondari hutatizika sana na kuona kama ni ukiukaji wa haki zao. Kisa kimojawapo ni kile ambacho wanafunzi Nyeri walifunga mabweni manne wakishutumu usimamizi kwa unyanyasaji tena usio wa haki. Wanafunzi wanne walipoteza maisha yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya (KESSHA), Indimuli Kahi, akiwa na baadhi ya walimu walishtumu Wizara ya Elimu kuwa imefeli katika jukumu lake la uangalizi ambalo lingesaidia katika kuepusha visa vya wanafunzi kuteketeza shule.

Utumiaji wa dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi shuleni, kulingana na mwenyekiti wa muungano wa walimu wa shule za sekondari na taasisi za juu (KUPPET) Omboko Milemba, ndio mojawapo ya sababu kuu za kutoridhika, na hivyo kufanya kutowezekana kwa walimu kuwaadhibu wanafunzi.

Shule zote zinapaswa kuwa na idara ya ushauri-nasaha ambayo iko tayari kila wakati kutoa usaidizi unaohitajika kwa wanafunzi.

Walimu, wazazi na wanafunzi wawe na uwezo wa kukusanyika pamoja na kuwasikiliza wanafunzi na kuwa na mazungumzo ya jinsi ya kutatua masuala muhimu yanayohusu shule.

You can share this post!

Kinaya kandarasi za EACC zikitiliwa shaka

Kibiwott Kandie na Peres Jepchirchir waendea mataji ya New...

T L