• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kigen ashindia Kenya medali ya kwanza Olimpiki

Kigen ashindia Kenya medali ya kwanza Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imepoteza taji la Olimpiki la mbio za wanaume za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa mara ya kwanza tangu 1984 baada ya kuridhika na nishani ya shaba kupitia Benjamin Kigen jijini Tokyo nchini Japan, Agosti 2.

Hii ni medali ya kwanza ya Kenya katika makala haya ya 32 tangu yaanze rasmi Julai 23.

Mmoroko Soufiane El Bakkali, ambaye amekuwa na msimu mzuri katika mbio hizo za kuruka viunzi mara 28 na maji mara saba, alinyakua dhahabu kwa dakika 8:08.90.

Medali ya fedha imenyakuliwa na Muethiopia Lamecha Girma (8:10.38) ambaye alikuwa ameongoza kwa muda mrefu kabla ya kupitwa na El Bakkali katika kona ya mwisho.

Kigen pia alielekea kona ya mwisho akiwa pabaya, lakini alijikakamua na kung’oa Muethiopia Getnet Wale katika nafasi ya tatu na kutwaa shaba kwa dakika 8:11.45, sekunde tatu mbele ya Wale.

Kabla ya kupoteza taji, Kenya ilikuwa imeshinda makala tisa mfululizo kupitia kwa Julius Korir (1984, Los Angeles), Julius Kariuki (Seoul, 1988), Matthew Birir (1992, Barcelona), Joseph Keter (1996, Atlanta), Reuben Kosgei (Sydney), Ezekiel Kemboi (2004 Athens na 2012 London), Brimin Kipruto (2008) na Conseslus Kipruto (2016).

Wakenya wengine waliowahi kunyakua dhahabu katika kitengo hiki ni Amos Biwott mwaka 1968 (Mexico) na Kipchoge Keino mwaka 1972 (Munich).

Ni mara ya kwanza kabisa Morocco imeshinda taji hilo tangu mbio za wanaume za 3,000 kuruka viunzi na maji zijumuishwe kwenye Olimpiki mwaka 1920.

  • Tags

You can share this post!

Kwa sasa Raila ndiye Naibu Rais – Murkomen

Obiri aridhika na medali ya fedha tena Olimpiki