• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Kwa sasa Raila ndiye Naibu Rais – Murkomen

Kwa sasa Raila ndiye Naibu Rais – Murkomen

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen amesema Naibu Rais William Ruto hafai kulaumiwa kwa makosa yaliyotendeka wakati wa muhula wa pili wa utawala wa Jubilee kwa sababu alitengwa.

Bw Murkomen ameongeza kuwa japo kisheria Dkt Ruto anasalia kuwa Naibu Rais, kiuhalisia majukumu ya afisi hiyo yanatekelezwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“William Ruto hafai kulaumiwa kwa yale yaliyofanyika katika serikali hii ndani ya miaka minne iliyopita kwa sababu yeye sio sehemu ya utawala huu. Yuko pale tu kwa misingi ya sheria lakini Naibu Rais halisi ni Raila Odinga,” akasema kwenye mahojiano katika Redio Spice FM.

Bw Murkomen alionekana kuendeleza kauli ambayo imekuwa ikitolewa na Dkt Ruto mwenyewe katika majukwaa mbalimbali kwamba mambo yalianza kuenda kombo serikali baada ya Bw Odinga kuingia serikalini kupitia handisheki mnamo Machi 9, 2018.

Majuma mawili yaliyopita Naibu Rais alilaumu Odinga viongozi wengine wa upinzani kwa sakata ya ufisadi iliyotokea katika Halmashauri ya Dawa Nchini (KEMSA) ambapo Sh7.8 bilioni zilipotea.

Pesa hizo zilipotea kupitia ununuzi wa vifaa vya kinga dhidi ya Covid-19 (PPEs) kwa bei ya juu kupita kiasi kupitia zabuni iliyotolewa kinyume cha sheria.

“Hao wanaozungumza kuhusu ufisadi ndio walifaidika kwa kuwapokonya wagonjwa wa corona dawa katika kile kinachotajwa kama Covid billionaires. Sisi tuliwekwa kando walipoingia serikalini kupitia handisheki lakini sasa wanatuonya kuhusu ufisadi,” Dkt Ruto akasema baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika mtaa wa Umoja 11, Nairobi.

Naibu Rais alikuwa akijibu tishio ambalo Bw Odinga alitoa akiwa Mombasa awali kwamba endapo atashinda urais 2022 atahakikisha washukiwa wote wa ufisadi wamesukumwa gerezani.

“Tukiunda serikali ijayo wezi wote wa mali ya umma kupitia ufisadi wamepeleke katika gereza la Shimo la Tewa. Hatutavumilia uovu kama huu ambao umedumaza maendeleo nchini,” Bw Odinga akasema alipokutana na viongozi wa ODM eneo bunge la Mvita mnamo Julai 2, 2021.

You can share this post!

Raila amezea mate OKA

Kigen ashindia Kenya medali ya kwanza Olimpiki