• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
Kikosi cha Hertha Berlin nchini Ujerumani chamtimua Jens Lehmann kwenye Bodi ya Usimamizi kwa sababu ya ubaguzi wa rangi

Kikosi cha Hertha Berlin nchini Ujerumani chamtimua Jens Lehmann kwenye Bodi ya Usimamizi kwa sababu ya ubaguzi wa rangi

Na MASHIRIKA

KIPA wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ujerumani, Jens Lehmann, 51, amepigwa kalamu katika Bodi ya Usimamizi ya klabu ya Hertha Berlin katika Ligi Kuu ya Ujerumani.

Hii ni baada ya mlinda-lango mstaafu kupatikana na hatia ya kuendeleza ubaguzi wa rangi kupitia mtandao wa kijamii. Akitumia mtandao wake wa WhatsApp, Lehmann alimtumia Dennis Aogo ambaye ni mchanganuzi wa soka wa Sky Sports nchini Ujerumani ujumbe akimwita “mtu mweusi”.

Aogo alipiga picha ujumbe huo baadaye na kuusambaza kupitia mtandao wa Instagram akisema, “Ala! Lehmann, huu kweli ni ujumbe wangu, nadhani ulikusudia kumtumia mtu tofauti.”

Hata hivyo, Lehmann alikiri kwamba alidhamiria ujumbe huo umfikie Aogo ambaye ni beki wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani.

Ingawa Lehmann aliomba radhi, kampuni ya uwekezaji ya Tennor Holding ambayo Lehmann alikuwa akiwakilisha kwenye Bodi ya Usimamizi ya Hertha pia imesema kwamba mkataba wa mlinda-lango huyo nayo umetamatishwa mara moja.

“Kauli za hiyo si sehemu ya utamaduni wetu na haziwakilishi maadili wala falsafa ya kikosi chetu,” akasema rais wa Hertha Berlin, Werner Gegenbauer.

“Tunajitenga na kauli hiyo ya Lehmann kwa kuwa matamshi yake hayawakilishi kwa vyovyote mtazamo au msimamo wa Tennor Holding kuhusu vita dhidi ya ubaguzi wa rangi. Tunaunga mkono hatua ya Hertha Berlin kumtimua Lehmann kwa kuwa nasi tumetamatisha kandarasi na kipa huyo mstaafu mara moja,” ikasema sehemu ya taarifa ya Tennor Holding.

Aogo, 34, aliwahi kuchezea Hamburg na Stuttgart katika Bundesliga na akawajibishwa na timu ya taifa ya Ujerumani mara 12 kabla ya kustaafu kwenye ulingo wa usogora mnamo Agosti 2020.

Kwa upande wake, Lehmann alichezea Arsenal mara 200 katika awamu mbili tofauti kabla ya kuangika glavu zake rasmi mnamo 2011.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uhuru, Raila wataka wabunge na maseneta kupitisha mswada wa...

Ni Chelsea na Manchester City kwenye fainali ya UEFA Mei 29