• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Kipa Courtois awaokoa Real Madrid dhidi ya Getafe kwenye gozi la La Liga

Kipa Courtois awaokoa Real Madrid dhidi ya Getafe kwenye gozi la La Liga

Na MASHIRIKA

KIPA Thibaut Courtois wa Real Madrid alifanya kazi ya ziada ya kupangua makombora mazito kutoka kwa wanasoka wa Getafe waliowalazimishia sare tasa katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumapili usiku.

Alama moja iliyotiwa kibindoni na Real katika mchuano huo iliwasaza katika nafasi ya pili jedwalini kwa pointi 67, tatu nyuma ya viongozi Atletico Madrid ya kocha Diego Simeone.

Hata hivyo, Real wanaotiwa makali na kocha Zinedine Zidane, sasa wako katika hatari ya kupitwa na Barcelona ambao wanafunga mduara wa tatu-bora kwa alama 65 huku wakiwa na mchuano mmoja zaidi wa kucheza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na washindani wao wakuu – Atletico, Real na Sevilla wanaoshikilia nafasi ya nne kwa alama 64.

Real walikosa huduma za idadi kubwa ya wanasoka wao tegemeo katika mechi dhidi ya Getafe kutokana na majeraha, marufuku na ugonjwa wa Covid-19.

Courtois alidhibiti vilivyo fataki ya fowadi Mathias Olivera mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya kumnyima mshambuliaji raia wa Ubelgiji, Nemanja Maksimovic, fursa nyingine ya wazi ya kufungia Getafe bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Nusura Vinicius Junior naye afungie Real goli muhimu mwanzoni kwa kipindi cha pili ila kombora lake likanyakwa na kipa David Soria aliyesalia bila kazi kubwa ya kufanya baada ya mabeki wa Getafe kuwazima kabisa mafowadi wa Real.

Real walishuka dimbani kwa ajili ya mchuano huo siku chache baada ya kukomoa Barcelona 2-1 katika gozi la El Clasico uwanjani Alfredo Di Stefano na kuwabandua Liverpool kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Leicester City walenga historia baada ya kufuzu kwa fainali...

Mamelodi anayochezea Mkenya Brian Mandela yapoteza ufalme...