• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Kipchoge aliyeshambuliwa kwa kimya kirefu asema hakushangaa kuona dogo Kelvin Kiptum akivunja rekodi yake

Kipchoge aliyeshambuliwa kwa kimya kirefu asema hakushangaa kuona dogo Kelvin Kiptum akivunja rekodi yake

LABAAN SHABAAN Na GEOFFREY ANENE

NGULI wa mbio za Marathon Eliud Kipchoge amesema ‘hakushangazwa’ na Mkenya mwenzake Kelvin Kiptum kuvunja rekodi ya dunia ya mbio hizo.

Kiptum alivunja rekodi ya marathon iliyoshikiliwa na Kipchoge alipotimka kwa saa mbili na sekunde 35 katika mashindano ya Chicago Marathon nchini Amerika mnamo Oktoba 8, 2023.

Alivunja rekodi ya Kipchoge ya saa 2:01:09 ya Berlin, Ujerumani iliyonakiliwa Septemba 25, 2022.

Baada ya Kiptum kushangaza dunia, baadhi ya Wakenya walimvamia Kipchoge kwa sababu hakusema chochote hadharani kuhusu dogo ‘aliyempokonya sifa’.

Sasa, lejendari wa mbio hizi amesema michezo si mashindano.

“Nimewaonyesha wa kizazi kipya njia ya kufuata. Nimevunja rekodi hizi mara mbili,” alisema Kipchoge ambaye aliongea kwa mara ya kwanza tangu Kiptum kung’aa.

Kipchoge ambaye ni mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia mbio hizo za umbali wa kilomita 42, mnamo Ijumaa alipokea tuzo ya kifahari ya Uhispania ya Binti Mfalme wa Asturias akiwa ni wa kwanza kushinda kitengo cha michezo kutoka Kenya.

Bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki alishinda tuzo hiyo ya kifalme ya mwaka 2023.

Amefuata nyayo za Mwingereza Sebastian Coe (mwaka 1987), ambaye sasa ni rais wa Shirikisho la Riadha Duniani, Mhispania Juan Antonio Samaranch (Olimpiki), Sergey Bubka kutoka Ukraine (riadha), Mwamerika Carl Lewis (riadha), raia wa Morocco Hicham El Guerrouj (riadha), Mjerumani Michael Schmacher (magari ya langalanga), Mhispania Rafael Nadal (tenisi) na Muethiopia Haile Gebreselassie (riadha), miongoni mwa wengine.

“Kupokea tuzo ya Uhispania ya Binti Mfalme wa Asturias ni heshima kubwa kwa sababu ni ithibati ya kitu nimekuwa nikiamini maisha yangu ya riadha. Kwa baadhi ya watu, mbio ni mwendo wa viungo. Lakini, tangu nianze kukimbia nikiwa mtoto mdogo mjini Kapsabet nchini Kenya, nilijua kuwa mbio ni zaidi ya mwendo wa mwili. Ni njia iliyo na nguvu za kutuunganisha,” Kipchoge alisema baada ya kupkea tuzo hiyo nchini Uhispania mnamo Oktoba 20.

Aliongeza, “Tunaweza kupata mafanikio makubwa ikiwa tutaamini kuwa hakuna kitu kinaweza kutushinda. Hakuna vizuizi isipokuwa akili yetu inavyotuchezea akili. Kwa hivyo nakuomba uone ulimwengu kwa njia hii. Kuona dunia bila ya vikwazo na kuona kuwa kila kitu kinawezekana. Dunia inayochukulia ukimbiaji kwa uzito ni dunia iliyo na furaha. Dunia inayotilia maanani ukimbiaji kwa uzito ni dunia iliyo na umoja.”

Alihutubia kikao hicho kilichoandaliwa na familia ya Kifalme siku chache baada ya kuzuru mji wa Shanghai nchini Uchina ambako pia alitumia fursa hiyo kupigia debe ukimbiaji kupitia kwa mradi wa INEOS 1:59 Pace Challenge.

  • Tags

You can share this post!

KCB RFC wapiga Oilers kujikatia tiketi ya fainali ya Impala...

Wanandoa wanaotaka kupata watoto wakatazwa kula samaki...

T L