• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 2:59 PM
Wanandoa wanaotaka kupata watoto wakatazwa kula samaki wakubwa

Wanandoa wanaotaka kupata watoto wakatazwa kula samaki wakubwa

NA ANGELINE OCHIENG

ULAJI wa samaki wakubwa unaweza ukapunguza uwezo wa kupata watoto miongoni mwa wanaume na wanawake, wataalamu wameonya.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Masuala ya Uzazi (IFFS) Oladapo Ashiru, samaki wakubwa wamegundulika kuwa na madini hatari yanayoweza kusababisha utasa na ugumba.

Mwaka 2017, utafiti wa Chuo cha Mafunzo ya Tiba cha Harvard ulibainisha kwamba samaki waliovuliwa kutoka maji makuu huwa na madini mazito ya Zebaki kwa sababu ya kuwala samaki wadogo.

Utafiti huo ulionya kwamba ulaji wa samaki wakubwa kama papa, samaki wa upanga, na samaki wengine ambao kwa Kiingereza hufahamika kama tilefish na King Mackerel, una athari mbaya kwa wanaotaka kupata watoto.

“Wanandoa wanaotaka kupata watoto wasile samaki wakubwa kwa sababu wana chembechembe za madini mazito na hatari kwa mfumo wa afya ya uzazi,” akasema Prof Ashiru.

Amesema ulaji wa samaki na viumbe wengine wa hatari bila ufahamu wa madini yaliyoko kwenye miili ya viumbe hao ni chanzo kipya cha baadhi ya watu kushindwa kupata watoto.

Aidha, Prof Ashiru aliwaonya wanawake dhidi ya kuendesha magari wakiwa miguu peku bila viatu.

“Mwanamke akikanyaga breki au klachi ya gari akiwa miguu tupu afahamu anajiweka kwa hatari ya madini mazito kuingia mwilini mwaka na kusababisha mimba kutoka au uwezo wa mimba kujitunga jinsi inavyofaa,” akaonya.

Mtaalamu huyo amewataka wanaume nao wazingatie lishe bora, akiwaonya walio na mazoea ya kula sukari mbadala kutoka kwa dawa aina ya Canderel kuwa inaweza ikapunguza mbegu zao za kiume.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kwamba ugumba na utasa mtawalia ni hali za mwanamume na mwanamke baada ya kipindi cha miezi 12 ya kuonana kimwili mara kwa mara bila kinga, wanakosa kabisa matokeo ya mimba kwa mwanamke.

Prof Ashiru akihutubu kwa makala ya 10 ya Merck Foundation Africa Asia Luminary 2023 mjini Mumbai, India kati ya Oktoba 18 na Oktoba 192023, alisema kutambua visababishi vya utasa ni muhimu.

Hafla hiyo ilivutia washiriki 6,000 kutoka kwa mataifa 70 ya bara Afrika na bara Asia.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Merck Foundation Dkt Rashja Kelej alisema hafla hiyo huwasaidia wataalamu kukutana ili kuchambua na kutafuta suluhu ya changamoto za kiafya kwa mataifa yao.

  • Tags

You can share this post!

Kipchoge aliyeshambuliwa kwa kimya kirefu asema hakushangaa...

Jinsi uharibifu wa Milima ya Shella unavyohatarisha Lamu...

T L