• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kipchoge azoa Sh7.4 milioni za tuzo ya Kihispania ya Binti Mfalme wa Asturias

Kipchoge azoa Sh7.4 milioni za tuzo ya Kihispania ya Binti Mfalme wa Asturias

Na GEOFFREY ANENE

GUNGE wa mbio za kilomita 42, Eliud Kipchoge amejizolea Sh7.4 milioni baada ya kushinda tuzo ya kifahari ya Uhispania ya Binti Mfalme wa Asturias kitengo cha michezo mwaka 2023.

Wakfu wa Uhispania unaoandaa tuzo hiyo ulisema Alhamisi kuwa Kipchoge ni shujaa katika ulimwengu wa riadha na ni bora duniani katika historia.

Kipchoge, ambaye atafikisha umri wa miaka 39 hapo Novemba 5, 2023, anajivunia kutwaa mataji mawili ya marathon kwenye Olimpiki.

Yuro 50,000 alizopewa ni moja ya tuzo katika vitengo vinane zinazotolewa na wakfu huo kwa kazi safi.

Tuzo hizo zinapeanwa kila mwaka na wakfu huo. Ni miongoni mwa tuzo za kifahari kabisa katika mataifa yanayozungumza Kihispania.

Mwigizaji Meryl Streep kutoka Amerika alitawazwa bora katika kitengo cha sanaa, mwanafalsafa na mwandishi wa vitabu Nuccio Ordine kutoka Italia (mawasiliano na wema) na mwanahistoria Hellene Carriere d’Encausse kutoka Ufaransa (sayansi za kijamii).

Washindi wa vitengo vya fasihi, ushirikiano wa kimataifa, utafiti wa kiufundi na sayansi pamoja na mapatano watatangazwa kati ya Mei 24 na Juni 14.

Bingwa wa marathon za Tokyo, London, Berlin na Chicago Kipchoge ameshinda tuzo nyingi zikiwemo mwanariadha bora wa Shirikisho la Riadha Duniani mwaka 2018 na 2019 na mchezaji bora mwanamume wa Chama cha Kamati za Kitaifa za Olimpiki (ANOC) wa michezo ya Olimpiki 2020 mjini Tokyo.

Pia, ni mshindi wa tuzo ya kifahari ya kitaifa ya Kenya (SOYA) mwaka 2019 na 2022 Kipchoge.

Baadhi ya washindi wa tuzo ya Binti Mfalme wa Asturias iliyoanzishwa mwaka 1981 wa kitengo cha michezo ni watimkaji Haile Gebrselassie na Hicham El Guerrouj, kipa Mhispania Iker Casillas, mpaishaji wa magari Carlos Sainz kutoka Uhispania na rais wa sasa wa Shirikisho la Riadha Duniani Sebastian Coe kutoka Ungereza.

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Raila aingilie kati na kuzima uhasama kati ya...

Shakahola: Wanahabari wanyimwa fursa kuangazia mazungumzo...

T L