• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Shakahola: Wanahabari wanyimwa fursa kuangazia mazungumzo baina ya kamati ya seneti na ile ya usalama

Shakahola: Wanahabari wanyimwa fursa kuangazia mazungumzo baina ya kamati ya seneti na ile ya usalama

ALEX KALAMA Na FARHIYA HUSSEIN 

WANAHABARI wamezuiwa kuangazia mazungumzo baina ya kamati mahususi ya seneti na ile ya usalama katika Kaunti ya Kilifi kutaka kufahamu ripoti inayofafanua kuhusu vifo vya watu katika mazingira tata na ambao walizikwa katika msitu wa Shakahola.

Mazungumzo hayo yalikuwa yanafanyika katika chumba cha mikutano katika ofisi ya kamishina wa kaunti ya Kilifi mnamo Ijumaa.

Wanahabari wa shirika la Nation Media Group ambao walikuwa wameingia katika chumba hicho cha mikutano ili kunasa mazungumzo hayo wamefurushwa dakika chache baada ya Seneta wa Tana River Danson Mungatana ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya seneti inayochunguza vifo vya watu Shakahola kuuliza maswali akitaka kuelewa kuhusu zile ripoti ambazo serikali ya kaunti iko nazo kufikia sasa kuhusiana na unyama huo.

Aidha kabla ya Kamishina wa Kaunti ya Kilifi Josphat Biwot, Kamanda wa polisi kaunti ya Kilifi Fatuma Ali, CCI wa Kaunti ya Kilifi, Mkuu wa Shirika la Ujasusi (NIS) katika Kaunti ya Kilifi na Kamanda wa Polisi wa Utawala (AP) wa Kaunti ya Kilifi kuanza kujibu maswali yaliyoulizwa na mwenyekiti wa kamati hiyo ya seneti wanahabari wameambiwa waondoke wakisema mkutano huo hauhitaji wanahabari.

Kamati ya seneti ambayo mnamo Ijumaa imezuru Kaunti ya Kilifi inataka kubaini nini hasa kilitokea.

Asubuhi Mungatana aliongoza wanachama wa kamati hiyo kutembelea makazi ya gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro ambapo ilifanya mkutano wa kwanza na kiongozi huyo kabla ya kuelekea kwa kamshina wa kaunti hiyo na inatarajiwa kufanya msururu wa mikutano na washikadau.

Kamati hiyo yenye wajumbe 11 inajaribu kubaini iwapo kulikuwa na ukiukaji wowote wa usalama katika eneo hilo, na kusababisha vifo hivyo.

Baadaye kamati hiyo itakutana na washiriki na waanzilishi wa Kanisa la Goodnews ambalo linahusishwa na mchungaji tata Paul Mackenzie na waathiriwa na familia zilizoathirika.

“Tunataka kuelewa jinsi vifo vya zaidi ya watu 200 vilitokea. Mshukiwa mkuu Mackenzie tayari amekamatwa lakini haiwezekani kwamba yeye bila bunduki alifanya hayo yote bila kusaidiwa na watu au asasi fulani. Ndicho tunachotaka kufahamu,” amesema seneta Mungatana.

Baadaye mchana, kamati hiyo imekutana na viongozi wa makanisa na taasisi mbalimbali za dini na wawakilishi wao, kabla ya kutembelea Msitu wa Shakahola kesho Jumamosi asubuhi.

Ziara hii itakuwa ya pili kwa kamati hiyo kushirikisha umma tangu iundwe wiki mbili zilizopita.

Mazungumzo ya kwanza yalikuwa ilipomuita Mwanasheria Mkuu Justin Muturi mbele yake. Ni mwanasheria mkuu ambaye afisi yake inawajibika kwa usajili na kanuni za taasisi za kidini.

Wakati wa mkutano wa wiki jana, Bw Muturi alikiri kwamba Kasisi Mackenzie na Kanisa la Newlife Church la Mchungaji Ezekiel Odero wamekiuka sheria na wanakabiliwa na uwezekano wa kufutiwa usajili.

Makanisa hayo mawili yamepewa notisi ya siku 30 kueleza kwa nini makanisa yao yasifungwe kwa kukiuka vifungu vya Sheria ya Vyama kufuatia mauaji ya Shakahola.

Mwanasheria mkuu aliendelea kusema kuwa udhaifu katika sheria na vikwazo vya bajeti umefanya karibu kushindwa kwa serikali kudhibiti ipasavyo taasisi za kidini.

Ingawa alielezea Sheria ya mashirika ya kijamii kuwa ni ya kizamani, “ya zamani na ya kawaida” alisema ugawaji mdogo wa bajeti kwa idara yake umefanya kuwa vigumu kwa ofisi ya msajili wa mashirika kufungua ofisi za kaunti ili kusimamia kikamilifu vitendo hivyo na kubana pale ambapo kuna ukiukwaji wa sheria.

  • Tags

You can share this post!

Kipchoge azoa Sh7.4 milioni za tuzo ya Kihispania ya Binti...

Arsenal kufika mwisho wa lami wakiteleza dhidi...

T L