• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Kipchoge, Kosgei wajitosa Tokyo Marathon

Kipchoge, Kosgei wajitosa Tokyo Marathon

Na GEOFFREY ANENE

Washikilizi wa rekodi za dunia mbio za kilomita 42 Eliud Kipchoge (saa 2:01:39) na Brigid Kosgei (2:14:04) watawania mataji ya Tokyo Marathon nchini Japan mnamo Machi 6.

Wenyeji walitangaza jana orodha ya majina makubwa yatakayoshiriki mbio hizo zinazorejea baada ya kukosa kufanyika 2021 kwa sababu ya janga la virusi vya corona. Kipchoge, 37, alitangaza Januari kuwa ndoto yake kabla ya kustaafu ni kutwaa mataji ya Marathon Kuu Duniani (WMM) – Tokyo, Boston, London, Berlin, Chicago, New York na Riadha za Dunia ama Olimpiki.

Anajivunia usuhindi wa Chicago (2014), Berlin (2015, 2017 na 2018) na London (2015, 2016, 2018 na 2019). Hajawahi kushiriki Tokyo, Boston wala New York tangu ajitose kwenye marathon mwaka 2013. Kipchoge alitawala marathon kwenye Olimpiki 2016 nchini Brazil na 2021 mjini Sapporo, Japan.

Jijini Tokyo, atapimwa vilivyo weledi wake na Waethiopia Birhanu Legese (2:02:48) na Mosinet Geremew (2:02:55), na Wakenya Amos Kipruto (2:03:30), Jonathan Korir (2:04:32) na Laban Korir (2:05:58), miongoni mwa wengine.

Bingwa mara mbili wa marathon za Chicago na London, Kosgei atawania umalkia wa Tokyo Marathon dhidi ya Mkenya Angela Tanui (2:17:57) na Muethiopia Ashete Bekere (2:18:18), miongoni wa wengine. Wakimbiaji 165 nyota (wanaume 128 na kinadada 37) wako katika orodha iliyotangazwa Februari 18.

You can share this post!

Chebet, Simiyu wang’ara riadha za Kisumu

Macho kwa Obiri akiendea mamilioni ya fedha Ras Al Khaimah...

T L