• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
AKILIMALI: Mfumaji vikapu hodari, mtunzaji mazingira aliyeajiri wanawake wengi

AKILIMALI: Mfumaji vikapu hodari, mtunzaji mazingira aliyeajiri wanawake wengi

Na HAWA ALI

SAFARI yake kama mjasiriamali mwanamke haijakuwa rahisi.

Rehema Adams alizaliwa na kulelewa katika kijiji kidogo cha Kabale, Rabai eneo la Kilifi.

Alipokuwa mdogo sana, mama yake alimfunza kufuma vikapu na kutengeneza shanga pamoja na mapambo ya vito huku babake akifanya kazi ya ukulima wa mananasi.

Wazazi wakeu wamekuwa misukumo mikuu kwake. Mamake Rehema alimfuza mbinu za ujasiriamali na misingi ya biashara.

Katika elimu yake yote, Rehema alijua kwamba njia pekee ya kutamatisha mukwamo wa umaskini ilikuwa ni kufanya bidii, na kuanza kupata pesa mapema iwezekanavyo. Hivyo basi, baada ya masomo ya sekondari, alianza kuuza mitumba kupitia akiba zake.

Baadaye alianza kutengeneza kwa mikono na kuuza mapambo ya vito kwa kutumia mbinu alizofunzwa na mamake.

“Niliyatengeneza mapambo hayo ya vito kutoka kwa matumbawe. Kisha nilipata hela za kutosha kunisitiri na pia za kuwasaidia wazazi wangu kulipa karo za ndugu zangu,” anasimulia.

Biashara ya mapambo haikumnogea sana Rehema, akageuza kibao ana kuanza kufuma vikapu. Alianza kupata wateja wengi haswa baada ya serikali kupiga marufuku mifuko ya plastiki nchini. Watu wengi hawakuwa na njia mbadala kwa mifuko ya plastiki.

“Niliamua kuungana na wanawake wenzangu kijijini ili kufuma vikapu na kuuza kwa bei nafuu. Wateja wengi walipenda vikapu vyetu na kuanza kuagizia kwa wingi. Kikapu kimoja tunauza kwa Sh300 na ni vya kudumu. Wakati mmoja tuliwahi kuuza vikapu 500, tuliunda Sh15,000 kwa mpigo,” alisema.

Kikundi hiki cha ufumaji vikapu kimewapa kazi wanawake 8. Ndoto yake ni kuwa mzalishaji mkuu wa bidhaa na huduma zisizodhuru mazingira katika maeneo ya Afrika Mashariki ifikapo mwaka wa 2028.

Wafanyikazi wake pamoja naye hutengeneza vikapu kwa kutumia mikono yao yenye kipaji, mmoja baada ya mwingine, kupitia teknolojia ya rahisi yenye mtindo usiotoa kaboni yoyote na unaosisitiza urembo asilia dhidi ya ukamilifu wa kimashine. Wametengeneza mbinu ya mtungo wa thamani kwa kuwatia motisha wakulima na wengine wanaotupa malighafi.

Katika safari hii yote, Rehema na wenzake wamejifunza mengi.

“Ili kuanzisha biashara, anzia ulicho nacho. Nimekuja kutambua kwamba ushauri na mifumo ya mitandao ni muhimu, na kwamba ni afadhali kuanza kwa kiwango kidogo. Mbinu unazozikuza unaposhinda changamoto za kustawisha biashara yako zina thamani kubwa kupindukia,” anashauri.

“Wanawake wengine bado wanadharau aina fulani za kazi. Wanasahau kwamba idadi kubwa ya biashara za kimataifa zenye fanaka zilianza kwa kiwango kidogo tu. Tukibadilisha fikira zetu, basi kila mwanamke atawezeshwa kote ulimwenguni. Kuna kiasi kikubwa cha nafasi za kiasili zinazotuzunguka na katika jamii zetu zinazoweza kubadilisha maisha yetu,” anaongeza.

You can share this post!

AKILIMALI: Jinsi vijana watatu Mathare Kaskazini...

Kisa cha Covid-19 chatishia kampeni ya wanaraga wa Afrika...