• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kivumbi kikali KWPL ikiingia raundi ya 17

Kivumbi kikali KWPL ikiingia raundi ya 17

NA AREGE RUTH

LIGI Kuu ya Wanawake nchini (KWPL), inaingia raundi ya 17 wikendi hii huku mechi sita zikipangwa kupigwa katika viwanja tofauti tofauti nchini.

Kesho Jumamosi, Kangemi Ladies FC watashuka dimbani dhidi ya Trans Nzoia Falcons FC katika uwanja wa shule ya upili ya wavulana ya Dagoretti High.

Ugani Moi jijini Kisumu, Kisumu All Starlets FC watamaliza shughuli ya siku dhidi ya mabingwa mara tatu KWPL Vihiga Queens.

Kwenye mechi hiyo, mshambulizi wa Kisumu Monica Etot na kiungo wa kati Janet Moraa Bundi wa Vihiga ndio wachezaji ambao wataangaziwa sana.

Etot ndiye mfungaji bora KWPL na mabao 13 sawa na mshambulizi wa Thika Queens Wendy Atieno ambaye anauguza jeraha.

Bundi kwa upande mwingine ana mabao saba. Hata hivyo, alifungia Vihiga bao la kipekee wikendi iliyopita dhidi ya Bunyore Starlets ugani Mumias Sports Complex katika Kaunti ya Kakamega.

Baada ya kipigo cha 3-0 dhidi wanajeshi wa Ulinzi Starlets kwenye mechi ya awali uwanjani Ulinzi Sports Complex, Nairobi,  mabingwa watetezi Thika Queens watakuwa na kibarua dhidi ya Wadadia FC ugani Stima Club jijini Nairobi mnamo Jumapili.

Kwingineko, Kayole Starlets wako mkiani kwenye msimo wa ligi na watagaragazana dhidi ya Zetech Sparks ugani Camp Toyoyo jijini Nairobi.

Kipa tegemeo wa Zetech Stella Mboya, hatakuwa kwenye kikosi cha kocha Bernard Kitolo baada ya kupata kadi nyekundu kwenye mechi kati ya Gaspo Women ugani Gems Cambridge, Rongai kaunti ya Kajiado mnamo Aprili, 8, 2023.

Nakuru City Queens watakuwa wanatafuta ushindi wao wa 10 msimu huu watakapo vaana na Ulinzi Starlets katika uwanja wa Maonyesho ya Kilimo (ASK) jijini Nakuru.

Gaspo Women watamaliza shughuli ya wikendi dhidi ya Bunyore Starlets ugani GEMS Cambridge.

  • Tags

You can share this post!

Ni mzaha tu, mke wa Samidoh si mjamzito

Ogolla apandishwa cheo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, CDF

T L