• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kocha Andriy Shevchenko aajiriwa na Genoa hadi 2024

Kocha Andriy Shevchenko aajiriwa na Genoa hadi 2024

Na MASHIRIKA

GENOA wanaoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A), wameteua Andriy Shevchenko kuwa kocha wao mpya kwa mkataba utakaotamatika rasmi mnamo 2024.

Fowadi huyo wa zamani wa AC Milan na Chelsea mwenye umri wa miaka 45 anajaza pengo la Davide Ballardini aliyefutwa kazi na Genoa mnamo Novemba 6, 2021.

Shevchenko aliongoza timu ya taifa ya Ukraine kutinga robo-fainali za Euro 2020 ambapo walipepetwa na Uingereza 4-0 jijini Roma, Italia. Kocha huyo alijiuzulu mnamo Agosti 2021, wiki chache baada ya kipute cha Euro 2020 kukamilika.

Kufikia sasa, Genoa wanashikilia nafasi ya 18 kwenye msimamo wa jedwali la Serie A baada ya kutandaza jumla ya mechi 12 na kushinda mchuano mmoja pekee.

Shevchenko aliyeangika daluga zake katika ulingo wa usogora mnamo 2012, ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Ukraine kwa mabao 48 kutokana na mechi 111.

Alianza kusakata soka ya kulipwa kambini mwa Dynamo Kiev nchini Ukraine kabla ya kujiunga na AC Milan ya Italia mnamo 1999. Akiwa Milan, alishinda mataji matano ya haiba kubwa likiwemo la Serie A na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Nyota huyo alitawazwa mshindi wa Ballon d’Or mnamo 2004.

Shevchenko alijiunga na Chelsea mnamo 2006 kwa kima cha Sh4.7 bilioni na akatwaa Kombe la FA na League Cup kabla ya kurejea Milan kwa mkopo mnamo 2008.

Aliondoka ugani Stamford Bridge mnamo 2009 na kurejea Dynamo Kiev waliomsajili upya.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ghasia zatawala sare ya Bandari na KK Homeboyz

Handiboli: Midume wa chuo Kikuu cha Kenyatta wafuzu gozi la...

T L