• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Kocha Brendan Rodgers amtunuka sifa fowadi Jamie Vardy

Kocha Brendan Rodgers amtunuka sifa fowadi Jamie Vardy

Na MASHIRIKA

KOCHA Brendan Rodgers alikuwa mwingi wa sifa kwa fowadi Jamie Vardy aliyeongoza waajiri wake kucharaza Wolves 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi ugani King Power.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kocha Bruno Lage kusimamia kambini mwa Wolves tangu aaminiwe fursa ya kuwa mrithi wa mikoba iliyoachwa na Nuno Espirito Santo aliyehamia Tottenham Hotspur.

Vardy alifunga bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo iliyokutanisha Leicester na Wolves baada ya kushirikiana vilivyo na Ricardo Pereira.

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 34, alipachika wavuni jumla ya mabao 17 katika kampeni za msimu wa 2020-21, yakiwemo mawili katika siku ya mwisho ya muhula huo dhidi ya Spurs.

“Angali na miaka miwili zaidi kwenye mkataba wake wa sasa na Leicester. Anaimarika kila msimu na matarajio yetu ni kwamba atasalia katika ubora wake kwa mara nyingine kwa kuwa ndiye fowadi wetu tegemeo,” akatanguliza Rodgers.

“Ni mchezaji wa haiba kubwa ambaye ni miongoni mwa washambulizi bora zaidi duniani kwa sasa,” akaongeza kocha huyo wa zamani wa Liverpool na Celtic.

Wolves wanaoanza kuzoea maisha chini ya kocha Lage, walipoteza nafasi kadhaa za kusawazisha kupitia Adama Traore anayehemewa pakubwa na Liverpool.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Watumiaji mitandao ya kijamii wataka haki itendeke kwa...

Tammy Abraham atua Italia kukamilisha uhamisho wake hadi AS...