• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kocha Jurgen Klopp asema hataondoka Liverpool kwa hiari iwapo hatatimuliwa

Kocha Jurgen Klopp asema hataondoka Liverpool kwa hiari iwapo hatatimuliwa

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp amesema hana mpango wowote wa kuondoka kambini mwa Liverpool iwapo hatalazimishwa kufunganya virago.

Hata hivyo, amewataka mashabiki wa kikosi hicho kujitayarisha kwa mabadiliko makubwa ugani Anfield mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23.

Klopp anatoa kauli hiyo baada ya waajiri wake kuanza kusajili msururu wa matokeo duni katika kampeni za muhula huu. Kufikia sasa, Liverpool wanakamata nafasi ya tisa kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) huku pengo la alama 10 likitamalaki kati yao na Manchester United wanaofunga mduara wa nne-bora.

“Huenda awe ni kocha ataondoka au mabadiliko hayo yashuhudiwe kikosini. Madiliko lazima yawepo japo sioni nikiagana na Liverpool iwapo sitafurushwa na mtu,” akasema mkufunzi huyo raia wa Ujerumani.

Kwa mujibu wa Klopp, Liverpool hawatamsajili mchezaji yeyote mwingine muhula huu wa Januari 2023 baada ya kujinasia huduma za fowadi mzoefu raia wa Uholanzi, Cody Gakpo. Kubwa zaidi katika mipango ya Liverpool ni kurefusha mikataba ya James Milner, Naby Keita, Alex Oxlade-Chamberlain na Roberto Firmino. Knadarasi za wanne hao zinatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Liverpool watakuwa wageni wa Wolverhampton Wanderers ugani Molineux usiku wa Januari 17, 2023 kwa mechi ya marudiano ya raundi ya tatu ya Kombe la FA baada ya kutoshana nguvu kwa sare ya 2-2 ugani Anfield mnamo Januari 7, 2023.

Tofauti na Wolves waliokomoa West Ham United 1-0 katika pambano lao lililopita ligini, Liverpool watakuwa na mtihani mgumu wa kujinyanyua baada ya Brighton kuwatandika 3-0 katika EPL ugani Amex wikendi.

Matokeo ya Wolves dhidi ya West Ham yalikomesha rekodi yao duni ya kutoshinda mechi nne mfululizo katika mashindano yote. Kikosi hicho ambacho kimeng’olewa kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA mara tatu pekee tangu 2016, sasa kinakamata nafasi ya 16 kwenye jedwali la EPL kwa alama 17 sawa na Leicester City na Leeds United.

Kichapo kutoka kwa Brighton kiliacha Liverpool katika nafasi ya tisa kwenye jedwali la EPL kwa pointi 28 sawa na Chelsea waliopepeta Crystal Palace 1-0 ugani Stamford Bridge, Jumapili.

Liverpool sasa hawajashinda mechi tatu mfululizo katika mashindano yote. Wamefungwa mabao manane katika kipindi hicho na hawajawahi kuondoka ugani bila kufungwa bao katika michuano saba.

Mabingwa hao watetezi wa Kombe la FA wamewahi kuondolewa kwenye raundi ya tatu ya kipute hicho mara moja pekee katika kipindi cha misimu 11 iliyopita. Hiyo ilikuwa mikononi mwa Wolves mnamo 2018-19, mwaka mmoja baada ya Wolves kuwadengua kwenye raundi ya nne mnamo 2016-17.

Tangu Wolves wapokeze Liverpool kichapo cha 2-1 katika Kombe la FA mnamo 2019 ugani Molineux, masogora wa Jurgen Klopp walishinda mechi saba mfululizo dhidi ya mbwa-mwitu hao katika EPL hadi walipoambulia sare mwezi huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Soka: Young City Academy yazamia kuzalisha na kukuza vipawa

Fahamu ni kwa nini unashauriwa kunywa maji mengi

T L