• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
Kocha Ralf Rangnick akataa majukumu mapya ya kuwa mshauri kambini mwa Man-United

Kocha Ralf Rangnick akataa majukumu mapya ya kuwa mshauri kambini mwa Man-United

Na MASHIRIKA

ALIYEKUWA kocha mshikilizi wa Manchester United, Ralf Rangnick, amekataa majukumu mapya ya kuwa mshauri wa benchi ya kiufundi kambini mwa mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Badala yake, mkufunzi huyo raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 63 atapania kumakinikia zaidi kibarua cha kutia makali timu ya taifa ya Austria.

Kazi ya ushauri ambayo Rangnick alitarajiwa kutekeleza ugani Old Trafford ilikuwa sehemu ya makubaliano yake na Man-United alipoaminiwa kushikilia mikoba ya kikosi hicho mnamo Disemba 2021 baada ya mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer kutimuliwa kwa sababu ya matokeo duni.

Nafasi ya Rangnick kambini mwa Man-United ilitwaliwa na Erik ten Hag mwishoni mwa msimu huu baada ya kocha huyo kuagana rasmi na Ajax ya Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie).

Alipoulizwa na wanahabari wiki hii kuhusu majukumu halisi ya Rangnick ugani Old Trafford na mpangilio wa jinsi watakavyofanya kazi, Ten Hag alisema maamuzi hayo yalikuwa ya usimamizi wa Man-United.

Ni kauli ambayo ilifasiriwa kufichua jinsi ambavyo Mholanzi huyo hakuwa tayari kushirikiana na Rangnick kambini mwa Man-United.

Rangnick alitambulishwa rasmi kwa wasimamizi, mashabiki na wachezaji wa timu ya taifa ya Austria mnamo Mei 29, 2022.

Chini ya Rangnick, Man-United walishinda asilimia 38 pekee ya mechi zao, hiyo ikiwa rekodi duni zaidi ya kikosi hicho chini ya kocha yeyote kwenye EPL katika kipindi cha miaka 50.

Licha ya matokeo hayo duni, Man-United walikamilisha kampeni zao za EPL katika nafasi ya sita jedwalini na hivyo kufuzu kwa soka ya Europa League mnamo 2022-23.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kwekwe abanwa kuhusu ukuta wa Sh24.9 milioni

Mbinu chafu zatishia uadilifu wa uchaguzi

T L