• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 6:30 PM
Mbinu chafu zatishia uadilifu wa uchaguzi

Mbinu chafu zatishia uadilifu wa uchaguzi

NA CHARLES WASONGA

HUKU kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 9 zikishika kasi, matumizi ya mbinu chafu za kusaka uungwaji mkono zinaharibu uadilifu wa zoezi hilo.

Miongoni mwa mbinu hizo ni mwenendo wa wanasiasa kuwalipa vijana ili kuwazomea wapinzani katika mikutano ya kisiasa, pamoja na kuharibu mabango yao. Pia kumeripotiwa visa kadhaa vya fujo katika baadhi ya maeneo nchini.

Mnamo Jumapili, Naibu Rais William Ruto alilalamikia kuharibiwa kwa bango lake la kampeni jijini Kisumu. Eneo hilo ni ngome ya kisiasa ya mgombea urais wa Azimio Raila Odinga, ambaye ndiye mpinzani mkuu wa Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9, 2022.

Chama cha ODM kilipuzilia mbali madai ya Dkt Ruto kikitaja kisa hicho kuwa la cha uhalifu: “Hicho ni kitendo cha uhalifu na wahusika wanafaa kusakwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa ODM, Oduor Ongwen.

Wiki iliyopita Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga pia alilalamikia kuharibiwa kwa mabango yake katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo, akielekeza lawama kwa wapinzani wake.

Kufuatia kuongezeka kwa visa hivyo vya hujuma, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ameonya kuwa atawachukulia hatua kali wahusika.

“Tume hii haitasita kuwachukulia hatua kali wawaniaji ambao watapatikana na hatia ya kuharibu mabango ya wenzao ama kushiriki vitendo vingine vinavyokiuka sheria,” Bw Chebukati akasema.

Kulingana na sehemu ya 13 ya Sheria ya Makosa ya Uchaguzi, mtu atakayepatikana na kosa la kuharibu mabango ya kampeni na kuhujumu kampeni za wapinzani atatozwa faini ya Sh500,000 au afungwe jela kwa miezi sita au adhabu zote mbili.

KUZOMEWA

Mnamo Mei 16, mgombea mwenza wa Bw Odinga Martha Karua, alizomewa katika Kaunti ya Kirinyaga kwenye mkutano aliouandaa kusherehekea kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo. Kitendo hicho pia ni kinyume cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi na kanuni ya mienendo ya uchaguzi.

Washukiwa sita walikamatwa kuhusiana na kisa hicho kilichotokea katika eneo bunge la Mwea.

Hali kama hiyo ilimpata Bi Karua katika vituo vichache alivyohutubia wananchi katika msururu wa kampeni zake katika eneo pana la Mlima Kenya.

Mnamo Machi 26, mkewe Bw Odinga, Ida Odinga alizomewa katika mkutano wa maombi katika Kaunti ya Meru na watu walioshukiwa kuchochewa kisiasa.

Siku chache kabla ya kisa hicho, Seneta wa Meru Mithika Linturi alikuwa na wakati mgumu kuwahutubia wafuasi wake mjini humo alipozomewa na kundi la vijana waliokuwa wakisifu mrengo wa Azimio.

BW Linturi anawania ugavana wa kaunti hiyo kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA)

GHASIA

Juzi, Gavana wa Siaya Cornel Rasanga alizomewa mjini Siaya na watu walioaminika kuwa wafuasi wa wapinzani wake.

Ghasia pia zimeanza kushuhudiwa kwenye kampeni katika maeneo mbalimbali ya nchi. Wiki mbili zilizopita makundi mawili yanayohusishwa na wawaniaji ugavana wa Kaunti ya Murang’a, Irungu Nyakera na Joseph Wairagu yalikabiliana katika eneo la Gaturi, ambapo watu 12 walijeruhiwa na magari ya wapinzani kuharibiwa.

Katika Kaunti ya Homa Bay, wafuasi wa wawaniaji wa ugavana Gladys Wanga na Evance Kidero walipigana wiki mbili zilizopita ambapo watu saba walijeruhiwa na mali ya thamani kubwa kuharibiwa.

Katika Kaunti ya Migori, Mbunge wa Suna Magharibi Peter Masara alishambuliwa mwezi uliopita na wafuasi wa mpinzani wake.

Katika Kaunti ya Kisii kumekuwa na visa vya ghasia baadhi ya wawaniaji viti wameshambuliwa kwa mawe.

Wanasiasa wanalaumiwa kwa kutumia makundi ya wahalifu kuhujumu kampeni za wapinzani wao.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Ralf Rangnick akataa majukumu mapya ya kuwa mshauri...

Jinsi unavyoweza kuhifadhi mboga na bidhaa za saladi kwenye...

T L