• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:09 AM
Kocha Unai Emery azamisha matumaini ya Arsenal katika soka ya Europa League

Kocha Unai Emery azamisha matumaini ya Arsenal katika soka ya Europa League

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Arsenal ya kutwaa taji la Europa League na kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao yalizamishwa na Villarreal ya Uhispania mnamo Alhamisi uwanjani Emirates, Uingereza.

Hii ni baada ya kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kulazimishiwa sare tasa na timu inayotiwa makali na mkufunzi Unai Emery na hatimaye kubanduliwa kwa jumla ya mabao 2-1.

Matokeo hayo yanamaanisha kwamba Arsenal kwa sasa watakosa fursa ya kunogesha soka ya bara Ulaya msimu ujao kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25.

Wakiwa wamepigwa 2-1 katika mkondo wa kwanza, Arsenal walishuka dimbani kwa ajili ya marudiano wakiwa na ulazima wa kusajili angalau ushindi wa 1-0 ili kufuzu kwa fainali ya Europa League ambayo kwa sasa itawakutanisha Manchester United ambao ni watani wao wakuu katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Villarreal.

Pierre-Emerick Aubameyang alishuhudia kombora lake likigonga mwamba katika mchuano huo ulioshuhudia nafasi chache zaidi za kufungana mabao baada ya Villarreal kuibana zaidi ngome na safu yao ya ulinzi kwa vipindi vyote viwili vya mchezo.

Nicolas Pepe na Emile Smith Rowe walipoteza pia nafasi mbili za wazi walizozipata katika kipindi cha pili.

Kinachowauma zaidi mashabiki wa Arsenal ni kwamba kubanduliwa kwao kwenye gozi la Europa League kulifanyika mikononi mwa kocha Emery aliyewahi kudhibiti yao kwa kipindi cha miezi 18 kabla ya kutimuliwa mnamo Novemba 2019 na nafasi yake kutwaliwa na Arteta aliyekuwa mkufunzi msaidizi wa Man-City.

Huku Man-United wakiwakomoa AS Roma kwa jumla ya mabao 8-5 kwenye nusu-fainali, nao Chelsea na Man-City wakitarajiwa kunogesha fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), kudenguliwa kwa Arsenal kunakomesha matumaini ya fainali zote mbili za soka ya bara Ulaya msimu huu kupambwa na vikosi vinne vya EPL.

Villarreal watamenyana na Man-United kwenye fainali ya Europa League itakayopigiwa katika uwanja wa Miejski jijini Gdansk, Poland mnamo Mei 26, 2021.

Kuondolewa kwa masogora wa Arteta kwenye Europa League ni pigo kubwa kwa Arsenal ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tisa kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 49 licha ya kuwa miongoni mwa vikosi 12 vilivyohusishwa katika kuunda kipute kipya cha European Super League (ESL) wiki chache zilizopita.

Licha ya kunogesha kipute cha Europa League kwa kipindi cha misimu minne mfululizo iliyopita, Arsenal hawakuwahi kukosa fursa ya kusakata soka ya bara Ulaya, hasa gozi la UEFA, chini ya kocha Arsene Wenger tangu msimu wa 1996-97.

Hiki ni kipindi kigumu zaidi kwa Arsenal ambao wanashuhudia rekodi mbovu katika historia yao tangu kutimuliwa kwa kocha George Graham mnamo Februari 1995.

Matumaini na matarajio ya mashabiki wa Arsenal yalikuwa juu zaidi mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21 baada ya Arteta kuongoza waajiri wake kupepeta Liverpool kwenye Community Shield mnamo Agosti, miezi chache baada ya kutia kapuni ufalme wa Kombe la FA.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Manchester United kuvaana na Villarreal kwenye fainali ya...

Lapsset kufunguliwa mapema kuliko jinsi ilivyotarajiwa