• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Kocha wa Kenya Morans Liz Mills atuzwa mpira wa dhahabu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza timu ya wanaume AfroBasket

Kocha wa Kenya Morans Liz Mills atuzwa mpira wa dhahabu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza timu ya wanaume AfroBasket

Na JOSEPH KANYI

KOCHA Mkuu wa Kenya Morans, Liz Mills ametuzwa na Shirikisho la Mpira wa Vikapu Duniani (FIBA) kwa kuwa kocha wa kwanza kabisa mwanamke kuongoza timu ya wanaume katika Kombe la Afrika (AfroBasket).

Raia huyo wa Australia alitunukiwa mpira wa dhahabu katika siku ya mwisho ya makala ya 30 yaliyokamilika Septemba 5 usiku baada ya Tunisia kutetea taji lao kwa kuzaba Ivory Coast 78-75 ukumbini Kigali nchini Rwanda.

Mills alichukua majukumu ya kocha wa Kenya Morans kutoka kwa Cliff Owuor aliyenyakuliwa na klabu ya APR nchini Rwanda mapema Februari 2021.

Mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 34 aliongoza Morans kufuzu kushiriki AfroBasket kwa mara ya kwanza tangu 1993 mwezi uo huo kutoka Kundi B lililokuwa na miamba Angola na Senegal na Msumbiji. Morans iliduwaza Angola 74-73 mwezi Februari jijini Kigali na kujikatia tiketi.

Katika AfroBasket jijini Kigali, Kenya ilifika robo-fainali baada ya kupiga Mali 72-66 katika mechi yake ya mwisho ya makundi. Ililemewa na Sudan Kusini 60-58 katika robo-fainali na kumaliza mashindano hayo ya mataifa 16 katioka nafasi ya 12.

“Historia mpya ya makocha wanawake kufanya kazi katika timu za taifa za wanaume iliandikishwa kupitia kwa Liz Mills. Yeye ni kocha wa kwanza kabisa kutia makali timu ya wanaume katika Kombe la Afrika,” FIBA ilisema katika taarifa yake na kumsifu kuwa mfano bora kwa wasichana na wanawake barani Afrika na duniani.

Jedwali la mwisho la AfroBasket 2021: 1.Tunisia, 2.Ivory Coast, 3.Senegal, 4.Cape Verde, 5.South Sudan, 6.Angola, 7.Uganda, 8.Guinea, 9.Nigeria, 10.Rwanda, 11.Egypt, 12.Kenya, 13.DR Congo, 14.Central Africa Republic, 15.Mali, 16.Cameroon.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

MMUST: Viongozi Magharibi wapuuza habari za kupotosha...

Wakewenza wakazia buda asali