• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Kocha wa Simba United apongeza vijana wake kwa kufaulu kushiriki michuano ya Daraja La Pili

Kocha wa Simba United apongeza vijana wake kwa kufaulu kushiriki michuano ya Daraja La Pili

Na JOHN KIMWERE

KOCHA wa Simba United, Livingstone Wanga amemimia wachezaji wake sifa tele baada ya kuibuka mabingwa wa mechi za Kundi A kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu uliokamilika.

Wanga amesema hayo baada ya kikosi hicho kuzaba Umul Qura FC kwa mabao 2-0 kwenye patashika ya kusisimua iliyopigiwa uga wa Shule ya Msingi ya Pangani, Nairobi.

Mchezo huo ulianza kwa kasi huku pande zote zikishusha soka safi kwenye juhudi za kuwinda mabao ingawa hata kama Simba United ingepoteza bado ingesalia kifua mbele ikiwa imewapiku wapinzani wao kwa alama mbili.

Kipindi cha kwanza mchezo huo ulikamilika sare tasa. Kipindi cha pili wachezaji wa Simba walirejea kivingine wakilenga kubeba ushindi wa pointi tatu. Elvis Chozia alifunga bao la kwanza kabla Mickey Onyango kuongezea bao la pili.

”Bila shaka ninashukuru wachezaji wangu kwa kazi nzuri walioshusha kwenye kampeni za msimu na kufanikiwa kuibuka mabingwa wa kipute hicho,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa wapo tayari kupandishwa ngazi kushiriki kipute cha Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao.

Kocha wa Simba United, Livingstone Wanga (kushoto) akizungumza na wachezaji wake kabla ya kushuka dimbani kukabili Umul Qura FC kwenye mechi ya Kundi A kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL). Simba ilishinda kwa mabao 2-0. PICHA  | JOHN KIMWERE

Pia alidokeza kuwa kampeni hizo msimu huu zilishuhudia ushindani mkali kinyume na ilivyotarajiwa.

Hata hivyo alikariri kuwa soka la Kenya linazidi kuimarika licha ya Shirikisho la mchezo huo kufungiwa kutoshiriki mashindano ya kimataifa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Simba imeibuka kidedea kwa kufikisha alama 53, nane mbele ya Umul Qura FC. Kwenye mfululizo wa matokeo ya kipute hicho, Escalators FC ilitoka nguvu sawa bao 1-1 na African Warriors nayo MacMillan FC ilisajili ufanisi wa mabao 2-0 mbele ya Uthiru Vision.

Ni wazi kwamba Simba United ilikutanishwa na mabingwa wa Kundi B, Kasi Kasi FC katika fainali kutafuta ubingwa wa kipute hicho kwa jumla.

Kwa mara nyingine AFC Leopards Youth iliyopigiwa chapuo kufanya kweli imeshindwa kujikatia tiketi ya kusonga mbele kufuata nyayo za wenzao ambao hushiriki Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF-PL).

  • Tags

You can share this post!

Kapaito aanza kutesa wapinzani katika Ligi Kuu ya Ethiopia

Okutoyi apigwa breki raundi ya pili tenisi ya Nottingham...

T L