• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kocha wa Soccer Assassins atuma onyo kwa Solasa

Kocha wa Soccer Assassins atuma onyo kwa Solasa

NA TOTO AREGE

KOCHA wa timu ya Soccer Assassins Nickson Muleri amesema lazima wapate ushindi dhidi ya Solasa Stima Queens katika mechi ya 21 ya Zoni A ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Divisheni ya Kwanza.

Mechi hiyo itachezwa ugani Chambiti Primary mjini Luanda kaunti ya Vihiga leo.

Muleri amesisitiza kuwa, ushindi utafufua matumaini yao ya kujiunga na Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) msimu ujao.

“Tulifanya mazoezi yetu ya mwisho leo (Jumanne) na wasichana wangu wako tayari kupambana dhidi ya Assassins. Tunataka ushindi kwenye mechi hii hakuna lingine,” alisema Muleri.

Assassins kufikia sasa wamecheza mechi 21 na wameshikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na alama 43, alama tano nyuma ya vinara wa ligi Bungoma Queens.

“Tulikuwa na uwezo wa kutwaa ubingwa mapema lakini, kutocheza dhidi ya Gene Queens katikati ya msimu kulituponza kutokana na changamoto za kifedha. Hili lilitufanya tupoteze alama tatu na mabao mawili,” aliongezea Muleri.

Mshambulizi wa timu hiyo Valary Nekesa, ndiye mfungaji bora Zoni B na mabao 21 kutokana na mechi 20.

Solasa nao wako kwenye hatari ya kushuka daraja katika nafasi ya tisa na alama 18. Wamecheza mechi 20, wakapata ushindi mara sita, sare tatu na  kupoteza mechi 11.

Raundi ya mwisho ya mechi za msimu wa 2022/23 itachezwa wikendi hii. Kibera Soccer Women ya Zoni B ndio timu ya pekee ambayo imejiunga na KWPL.

Kwa upande mwingine, msimu ujao wa 2023/2024 Shirikisho la Soka nchini (FKF) limetangaza kuongeza ligi nyingine ya wanawake.

Kando na ligi KWPL na ya divisheni ya kwanza, Ligi Kuu ya Taifa (WNSL) itaanzishwa rasmi msimu ujao.

Dirisha la uhamisho lilifunguliwa rasmi tarehe 21 mwezi huu na litafungwa rasmi Septemba 29, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Kizaazaa demu akimpokonya polisi bunduki ndani ya...

Uwanja wa shule ya Gatina kukarabatiwa kwa Sh23 milioni

T L