• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kocha William Muluya aamini chipukizi wa Kariobangi Sharks watatesa ligini

Kocha William Muluya aamini chipukizi wa Kariobangi Sharks watatesa ligini

NA JOHN KIMWERE 

KOCHA mkuu wa Kariobangi Sharks, William Muluya anaamini kuwa kikosi chake cha wachezaji chipukizi kitafanya kweli kwenye kampeni za Ligi Kuu Kenya (FKF-PL) muhula huu.

Sharks ilipoteza takribani wanasoka 24 mwanzoni mwa muhula huu hali iliyochangia kuwapa nafasi wachezaji chipukizi  badala ya kusaini wengine wapya.

Kocha huyo anahisi kuwa chipukizi hao wanatosha mboga kukabili wapinzani wao kwenye ngarambe ya muhula huu.

”Sio siri tulipoteza wachezaji wengi wazuri lakini tuliamua kuwapa nafasi chipukizi wa timu ndogo ambapo tayari tumegundua wana uelewa mzuri,” anasema.

Anaongeza kuwa hatua hiyo inawatia moyo wachezaji wengine kukaza buti zaidi wakilenga kutwaa nafasi za wenzao wakipata makao mapya.

Sharks ilipoteza wachezaji muhimu akiwamo Patillah Omotto (Kenya Police), Enock Wanyama, Ziyad Kiwanuka, mnyakaji Brian Olang’o, Boniface ‘Kajos’ Onyango, Tom Teka na Eric Mmata aliyejiunga na Tusker FC.

Kati ya mechi saba ambazo imeshiriki imeshinda moja na kutoka nguvu sawa mara nne kisha kupoteza patashika mbili.

Kesho Jumatano, Januari 18, 2023, kikosi hicho kitashuka ugani Kasarani Annex kukaribisha Vihiga Bullets.

Kwenye msimamo wa mechi hizo, Sharks inashikilia nafasi ya 13 kwa alama saba, sawa na Wazito FC pia FC Talanta.

  • Tags

You can share this post!

Wazazi wa gredi ya 6 wapumua

Soka: Young City Academy yazamia kuzalisha na kukuza vipawa

T L