• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Argentina yaizidi maarifa Ufaransa kupitia penalti

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Argentina yaizidi maarifa Ufaransa kupitia penalti

CHRIS ADUNGO Na GEOFFREY ANENE

ARGENTINA ndio wafalme wapya wa soka duniani baada ya kufunga Ufaransa penalti 4-2 kufuatia sare ya 3-3 mwishoni mwa dakika 120 katika fainali iliyochezewa ugani Lusail Iconic, Qatar.

Ilikuwa mara ya tatu katika historia kwa bingwa wa dunia kuamuliwa kupitia penalti. Wafalme mara tano Brazil walitwaa ubingwa wa 1994 kwa kufunga Italia 3-2 baada ya sare tasa. Italia nao walipepeta Ufaransa 5-3 mnamo 2006 baada ya sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa ziada.

Mwaka huu, Lionel Messi aliweka Argentina kifua mbele kupitia penalti katika dakika ya 23 baada ya Ousmane Dembele kumwangusha Angel Di Maria ndani ya kijisanduku. Di Maria alipachika wavuni bao la pili la Argentina baada ya kushirikiana vilivyo na Alexis Mac Allister katika dakika ya 36.

Hata hivyo, Kylian Mbappe alirejesha Ufaransa mchezoni kupitia penalti ya dakika ya 80, sekunde 37 kabla ya kusawazisha kupitia krosi ya Marcos Thuram. Penalti hiyo ilisababishwa na Nicolas Otamendi aliyemkabili Randal Kolo Muani visivyo ndani ya kijisanduku.

Messi alirejesha Argentina uongozini katika dakika ya 108 kabla ya Mbappe kufunga penalti ya kusawazisha dakika mbili kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa. Mbappe aliibuka mfungaji bora wa fainali za mwaka huu nchini Qatar baada ya kupachika wavuni magoli manane.

Baada ya muda wa ziada kukatika, Argentina walipachika wavuni penalti nne kupitia kwa Messi, Paulo Dybala, Leandro Paredes na Gonzalo Montiel. Ufaransa walifunga mikwaju yao kupitia kwa Mbappe na Kolo Muani. Kipa matata wa Argentina, Emiliano Martinez, alipangua penalti ya Kingsley Coman huku Aurelien Djani Tchouameni akiupiga nje mkwaju wake.

Ushindi wa Argentina uliwafanya kuwa kikosi cha kwanza baada ya Uhispania mnamo 2010 kuwahi kujizolea Kombe la Dunia baada ya kupoteza mechi ya ufunguzi kwenye fainali za kipute hicho.

Ufaransa waliokomoa Croatia 4-2 kwenye fainali ya 2018 nchini Urusi, walionekana kulemewa katika takriban kila idara hadi walipoleta ugani wavamizi Marcus Thuram na Randal Kolo Muani kujaza nafasi za Olivier Giroud na Demebele mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Fainali za mwaka huu zilikuwa za tano na za mwisho kwa Messi ambaye ni kigogo wa Paris Saint-Germain (PSG) kunogesha kwenye Kombe la Dunia akivalia jezi za Argentina. Kombe la Dunia ndilo taji la pekee ambalo mshindi huyo mara saba wa Ballon d’Or alikuwa akikosa katika historia yake ya usogora.

Argentina sasa ni mabingwa mara tatu wa dunia. Waliwahi pia kunyanyua ufalme mnamo 1978 na 1986.Walijikatia tiketi ya kuelekea Qatar mwaka huu bila kupoteza mechi yoyote katika hatua za mchujo. Waliambulia nafasi ya pili katika Kombe la Dunia mnamo 1990 na 2014 baada ya kuchapwa 1-0 na Ujerumani nchini Italia na Brazil mtawalia.

Argentina waliofungua Kundi C kwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Saudi Arabia, walinyanyuka upesi na kulaza Mexico na Poland 2-0 kabla ya kupiga Australia 2-1 katika raundi ya 16-bora. Walifunga Uholanzi penalti 4-3 baada ya sare ya 2-2 katika robo-fainali kabla ya kunyuka Croatia 3-0 katika nusu-fainali.

Ufaransa ambao ni mabingwa mara mbili wa dunia (1998, 2018) walianza kampeni za Kundi D kwa ushindi wa 4-1 dhidi ya Australia kabla ya Tunisia kuwaduwaza 1-0 baada ya kucharaza Denmark 2-1. Waling’oa Poland katika raundi ya 16-bora kwa 3-1 kabla ya kuzima Uingereza 2-1 katika robo-fainali na kupepeta Morocco 2-0 katika hatua ya nne-bora.

Mechi ya fainali imefuatiliwa na watu wengi kote duniani.

Waziri wa Michezo wa Kenya, Ababu Namwamba alifika nchini Qatar kushuhudia mabingwa mara mbili Ufaransa na Argentina wakimenyana katika fainali hiyo iliyoanza Jumapili saa kumi na mbili jioni.

Taarifa kutoka Wizara ya Michezo zilisema kuwa Namwamba aliandamana na Katibu kutoka wizara hiyo Jonathan Mueke.

“Watahudhuria fainali hiyo kupata ujuzi na kufanya uchunguzi muhimu kama sehemu ya mipango ya kufufua soka ya Kenya,” taarifa zikasema.

Wawili hao wamekutana na Balozi wa Kenya nchini Qatar Boniface Mwilu.

Aidha, Namwamba alifichua mapema Jumapili kukutana na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Multichoice Africa, Fhulu Badugela kuhusu uwezekano wa SuperSport kurejea katika soko ya Kenya kupeperusha michezo na pia kuongeza vipindi vya sanaa katika runinga za Multichoice kama Maisha Magic.

Mabingwa wa dunia 1978 na 1986 Argentina wamekabana koo na wafalme wa 1998 na 2018 Ufaransa.

Macho yatmekuwa kwa washambulizi Lionel Messi (Argentina) na Kylian Mbappe (Ufaransa) ambao huchezea Paris Saint-Germain ya Ufaransa na wote wameonyesha umahiri wao.

You can share this post!

KPA waridhika nambari sita Afrika mpira wa vikapu

Wandayi awataka wakosoaji wa Raila ngomeni Luo Nyanza...

T L