• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 6:50 AM
Wandayi awataka wakosoaji wa Raila ngomeni Luo Nyanza wafyate au waunde chama

Wandayi awataka wakosoaji wa Raila ngomeni Luo Nyanza wafyate au waunde chama

NA CHARLES WASONGA

BAADHI ya wanasiasa kutoka Luo Nyanza sasa wanawataka wenzao walioasi ODM kukoma kumshambulia kiongozi wa chama hicho Raila Odinga la sivyo wagure chama hicho.

Kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi amesema uasi wa kisiasa unaotokota katika eneo hilo utavunjwa kabisa.

Bw Wandayi,  ambaye ni Mbunge wa Ugunja, amewaambia wanasiasa wa Luo Nyanza ambao hawajaridhishwa na uongozi wa ODM Bw Odinga kujiondoa polepole na kuunda chama chao.

“Tunataka kuwahakikishia kuwa uasi wowote utavunjwavunjwa inavyohitajika. Ikiwa unadhani kwamba una uwezo unda chama chako,” Wandayi akasema.

Alikuwa akiongea katika hafla ya mazishi ya marehemu Mama Rosa Amoth katika kijiji cha Pap Boro, eneobunge la Alego Usonga, kaunti ya Siaya.

Marehemu ni mamake Kaimu Mkurugenzi wa Afya Dkt Patrick Amoth na Gavana wa zamani wa Siaya Cornel Rasanga Amoth.

Kauli ya Bw Wandayi imeungwa mkono na Gavana wa Siaya James Orengo ambaye amesisitiza kuwa Bw Odinga sharti aheshimiwe.

“Hatutakubali watu wachache kumhujumu Raila Odinga. Viongozi wa ngazi za serikali ya kitaifa na wale wa serikali za kaunti wanafaa kumheshimu,” Orengo akasema.

Gavana Orengo amesema hakuna pengo la uongozi wa kisiasa katika eneo la Luo Nyanza huku akiwashauri wale ambao wanatafuta vinono kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza “kufanya hivyo kwa heshima.”

“Tunataka kufanya kazi pamoja ili kuleta maendeleo katika kila pembe ya nchi hii. Hata hivyo, ushirikiano huo kati ya Serikali ya Kitaifa na serikali za kaunti sharti ufanywe kwa kuzingatia mwongozo uliowekwa na Katiba,” Gavana Orengo akafafanua.

Tangu Bw Odinga alipopoteza katika uchaguzi wa urais Agosti 9, 2022 baadhi ya wanasiasa kutoka Luo Nyanza na Magharibi mwa Kenya wamegeuza miegemeo yao na kuamua kuegemea mrengo wa serikali ya Kenya Kwanza.

Aidha, wamedai muda wa Bw Odinga kustaafu kutoka siasa umetimu baada ya kufeli kutwaa kiti hicho baada ya majaribio matano.

Miongoni mwa wanasiasa hao ni aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero, aliyekuwa Mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo, aliyekuwa Mbunge wa Rangwe Martin Ogindo, aliyekuwa Mbunge wa Kabondo Kasipul Sylvance Osele, miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Argentina yaizidi maarifa...

Naibei, Jepchirchir watawala Iten Marathon, watia mfukoni...

T L