• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Nahodha Luka Modric kuendelea kuchezea Croatia hadi Juni-Julai 2023 baada ya kutwaa shaba ya Kombe la Dunia

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Nahodha Luka Modric kuendelea kuchezea Croatia hadi Juni-Julai 2023 baada ya kutwaa shaba ya Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

NAHODHA Luka Modric ana mipango ya kuendelea kusakata soka ya kimataifa hadi mwishoni mwa fainali za Uefa Nations League mnamo Juni 2023 baada ya kusaidia timu yake ya taifa ya Croatia kuambulia nafasi ya tatu katika Kombe la Dunia mwaka huu nchini Qatar.

Kiungo huyo wa Real Madrid mwenye umri wa miaka 37, alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kilichotegemewa na Croatia kupepeta Morocco 2-1 mnamo Jumamosi ugani Khalifa International katika mechi ya kutafuta mshindi nambari tatu na nne.

Alipoulizwa iwapo analenga kuendelea kucheza zaidi hadi fainali za Euro 2024, Modric alisema: “Tutaona hayo ila muhimu kwenda hatua kwa hatua. Nafurahia kuchezea timu yangu ya taifa,” akasema mshindi huyo mara moja wa taji la Ballon d’Or ambalo hutolewa kila mwaka wa mwanasoka bora zaidi duniani.

Modric alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Croatia katika mechi zote saba zilizotandazwa na wanafainali hao wa Kombe la Dunia 2018 nchini Qatar. Aliwajibishwa kwa dakika 656 kati ya 690 na anahisi kuwa angali na makuu zaidi ambayo anaweza kuipa timu yake ya taifa.

Croatia waliambulia nafasi ya pili duniani mnamo 2018 baada ya Ufaransa kuwapepeta 4-2 jijini Moscow, Urusi. Sasa wamemaliza fainali za Kombe la Dunia ndani ya mduara wa tatu-bora kwa mara ya tatu katika historia. Waliwahi kupepeta Uholanzi 2-1 mnamo 1998 nchini Ufaransa na kujizolea shaba nyingine.

Mabao yao dhidi ya Morocco yalifumwa wavuni kupitia Josko Gvardiol na Mislav Orsic. Walitinga nne-bora baada ya kufunga Brazil penalti 4-2 kufuatia sare ya 1-1 katika robo-fainali. Walifunga Japan penalti 3-1 baada ya sare ya 1-1 katika raundi ya 16-bora. Walicharaza Canada 4-1 baada ya kupiga sare tasa dhidi ya Morocco kisha kutoshana nguvu na Ubelgiji kwa sare tasa katika mechi za Kundi F.

Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu zilikuwa za mwisho kwa baadhi ya masogora wengi wa Croatia, akiwemo Luka Modric ambaye atakuwa na umri wa miaka 41 makala yakayo ya 23 ya Kombe la Dunia yatakapofanyika Amerika, Canada na Mexico.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Naibei, Jepchirchir watawala Iten Marathon, watia mfukoni...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Jinsi Croatia walivyoridhika na...

T L