• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
KOMBE LA DUNIA: Kibarua kizito kwa vikosi vya Afrika nchini Qatar

KOMBE LA DUNIA: Kibarua kizito kwa vikosi vya Afrika nchini Qatar

Na MASHIRIKA

BLACK Stars kutoka Ghana watapania kulipiza kisasi dhidi ya Uruguay baada ya vikosi hivyo kutiwa katika kundi moja kwenye makala ya 22 ya fainali za Kombe la Dunia zitakazochezewa nchini Qatar kati ya Novemba 21 na Disemba 18, 2022.

Gozi kati ya wawili hao katika Kundi H linalojumuisha pia Ureno na Korea Kusini, litarejesha kumbukumbu za robo-fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mnamo 2010. Wakati huo, Ghana walidenguliwa na Uruguay ambao ni mabingwa mara mbili wa dunia kupitia penalti 4-2 baada ya kuambulia sare ya 1-1 chini ya dakika 120.

Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia matuta fowadi Asamoah Gyan alipopoteza penalti mwishoni mwa muda wa ziada baada ya Luiz Suarez kunawa mpira ndani ya kijisanduku na kuonyeshwa kadi nyekundu. “Itakuwa fursa nzuri ya kulipiza kisasi dhidi ya Uruguay. Tulikuwa tumewashinda mnamo 2010 katika hatua muhimu lakini Suarez akatunyima nafasi ya kuandikisha historia. Tukio hilo, ambalo lingali bichi akilini mwetu, litatuchochea kuwazamisha,” akasema rais wa Shirikisho la Soka la Ghana, Kurt Okraku.

Suarez, 35, sasa anasakatia Atletico Madrid na amewahi pia kuvalia jezi za Liverpool na Barcelona. Huku akiwa bado sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Uruguay nchini Qatar, Ghana haitakuwa na mchezaji yeyote aliyejiunga timu yao miaka 12 iliyopita. Ghana wanaoshikilia nafasi ya 60 kimataifa, wanarejea kunogensha Kombe la Dunia baada ya kukosa makala ya 2018 na watafungua kampeni za Kundi H dhidi ya Ureno walioibuka wafalme wa bara Ulaya mnamo 2016.

Washikilizi wa Kombe la Afrika (AFCON), Senegal, watavaana na wenyeji Qatar katika Kundi A linalojumuisha pia Ecuador na Uholanzi ambao wamelemewa kwenye fainali mara tatu – 1974, 1978 na 2010. Senegal almaarufu Teranga Lions, wameshikilia nafasi ya kwanza barani Afrika kwa miaka mitatu iliyopita. Walinyanyua taji la AFCON kwa mara ya kwanza mnamo Januari 2022 walipopepeta Misri kwa penalti 4-2 baada ya sare tasa mwishoni mwa muda wa ziada.

The Atlas Lions wa Morocco watafungua kampeni zao za Kundi F dhidi ya Croatia waliopigwa na Ufaransa 4-2 kwenye fainali ya 2018 nchini Urusi. Kundi hilo linajumuisha pia Ubelgiji wanaoshikilia nafasi ya pili kimataifa kwa mujibu wa viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Canada ambao wamefuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1986.

The Carthage Eagles wa Tunisia wametiwa katika Kundi D pamoja na Denmark na mabingwa watetezi Ufaransa. Watapepetana pia na mshindi wa mchujo wa mwisho wa mabara ambaye atakuwa ama Peru, Australia au Falme za Milki ya Kiarabu (UAE). Cameroon wamepangwa katika Kundi G pamoja na mabingwa mara tano wa dunia, Brazil, ambao wamewahi kuwakomoa mara mbili katika makala ya awali ya Kombe la Dunia – 3-0 mnamo 1994 nchini Amerika na 4-1 mnamo 2014 nchini Brazil.

The Indomitable Lions wa Cameroon watakakuwa wakiwakilisha Afrika duniani kwa mara ya nane. Watavaana pia na Serbia na Uswisi watakaofungua nao kampeni za makundi. Ni mataifa matatu pekee kutoka Afrika ambayo yamewahi kutinga robo-fainali za Kombe la Dunia – Cameroon (1990), Senegal (2002) na Ghana (2010).

“Tumetiwa katika kundi gumu. Lakini tufanyeje? Croatia walitinga fainali mnamo 2018 nao Ubelgiji ni wa pili duniani. Hata hivyo, nafuu ni kwamba nafahamu fainali za Kombe la Dunia zilivyo. Chochote kinaweza kufanyika. Niliwahi kuongoza Algeria hadi raundi ya pili mnamo 2014 na nusura tushinde Ujerumani walioishia kutawazwa mabingwa,” akasema kocha wa Morocco, Vahid Halilhodzic.

Kwa upande wake, fowadi wa zamani wa Nigeria, Efan Ekoku alisema: “Senegal wapo pazuri kusonga mbele zaidi ya robo-fainali. Ndicho kikosi bora Afrika kwa miaka mitano iliyopita. Wanajivunia fowadi matata Sadio Mane, kipa wa haiba Edouard Mendy na beki mahiri Kalidou Koulibaly. Watatikisa dunia!”

DROO YA KOMBE LA DUNIA 2022:

KUNDI A: Qatar, Ecuador, Senegal, Uholanzi

KUNDI B: Uingereza, Iran, USA, Ukraine/Scotland vs Wales

KUNDI C: Argentina, Saudi Arabia, Mexico, Poland

KUNDI D: Ufaransa, Denmark, Tunisia, Australia/UAE vs Peru

KUNDI E: Uhispania, Ujerumani, Japan, Costa Rica/New Zealand

KUNDI F: Ubelgiji, Canada, Morocco, Croatia

KUNDI G: Brazil, Serbia, Uswisi, Cameroon

KUNDI H: Ureno, Ghana, Uruguay, Korea Kusini

You can share this post!

Harry Kane afikia rekodi ya Sergio Aguero kwa kunyanyua...

Raila: Niliponea shambulio la helikopta

T L