• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 10:50 AM
Raila: Niliponea shambulio la helikopta

Raila: Niliponea shambulio la helikopta

CHARLES WASONGA NA TITUS OMINDE NA ONYANGO K’ONYANGO

TASWIRA kamili ya tukio ambapo helikopta iliyombeba kiongozi wa ODM, Raila Odinga na ujumbe wake ilirushiwa mawe katika eneo bunge la Soy, kaunti ya Uasin Gishu ilianza kujitokeza huku Bw Odinga akidai vijana waliomrushia mawe walinuia kumuua.

Polisi wanasema ghasia zilizosababisha ndege hiyo kuharibiwa zilikuwa zimepangwa na baadhi ya viongozi. Bw Odinga na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed wamesimulia yaliyowafika wakati waziri mkuu huyo wa zamani alikuwa ameenda kuhudhuria mazishi ya Mzee Jackson Kibor katika kijiji cha Kebenes, eneo bunge la Soy, kaunti ya Uasin Gishu.

“Leo (Ijumaa) nusra tuuawe katika eneo bunge la Soy, kaunti ya Uasin Gishu, wakati wa mazishi ya Mzee Jackson Kibor. Helikopta yetu iliharibiwa kabisa na ilibidi tutafute chombo kingine cha usafiri,” akasema Bw Mohamed ambaye ni miongoni mwa walioandamana na Bw Odinga kufariji familia ya mwendazake.

Baadaye kwenye mahojiano na runinga ya Citizen usiku, Mbunge huyo wa Suna Mashariki alielezea jinsi magari yao yalivyoshambuliwa kwa mawe wakielekea kuabiri helikopta hatua chache kutoka kwa boma la Mzee Kibor.

“Hata hivyo, tuliweza kufika mahali ambapo helikopta yetu ilikuwa ikitusubiri. Lakini vijana hao ambao walionekana kukodiwa waliendelea kushambulia magari yetu kwa mawe kiasi kwamba, baadhi yetu tulishindwa kushuka,” Bw Mohamed akasema.

“Tulifaulu kuabiri helikopta na hata kabla ya kufunga mikanda, vijana hao waliendelea kuishambulia kwa mawe. Jiwe moja liligonga kioo cha helikopta upande ambapo Bw Odinga alikuwa ameketi,” akaongeza mbunge huyo, ambaye ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa.

Akasema: “Leo (Ijumaa) tungeuawa. Lakini Mungu alikuwa nasi. Walitaka kutuangamiza kabisa”.

Mbunge huyo alisema hawakujeruhiwa katika patashika hiyo ambayo ilidumu kwa muda wa karibu dakika 20 huku akikadiria idadi ya vijana waliowashambuliwa kuwa kati ya 300 na 500. “Japo, hatukujeruhiwa, hatukufahamu hali ya walinzi wetu ambao walisalia nyuma na wakasafiri kwa gari hadi mjini Eldoret.

Bw Mohamed, ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Odinga, alisema waliwasili katika boma la Mzee Kibor majira ya saa kumi jioni baada ya ibada ya mazishi kukamilika.

Awali, Bw Odinga ambaye ni mgombeaji urais wa muungano wa Azimio la Umoja aliendesha kampeni za kujipigia debe katika kaunti ya Iten ambako alizomewa na wafuasi wa Naibu Rais William Ruto.

“Tuliwasili katika boma la Mzee Kibor baada ya mazishi kukamilika. Tuliingia ndani ya nyumba na tukapata familia ya mwendazake. Pia walikuwepo Mbunge wa eneo hilo Caleb Kositany na Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago,” Bw Mohamed akasema.

Jana, Bw Odinga alielezea hatari iliyomfika Uasin Gishu Ijumaa akisema nia ya vijana hao ilikuwa ni kuwaangamiza kabisa.

“Sisi tulienda kutoa pole zetu kwa familia ya rafiki yangu Mzee Kibor Ijumaa lakini wakaanza kushambulia magari yetu kwa mawe. Vijana hao walitufuata hadi kwa ndege yetu na kuendelea kutushambulia. Mmoja wao alirusha jiwe kubwa kwenye kioo cha upande ambao nilikuwa nimeketi,” akasema.

“Kwa ukweli, watu hao walitaka kutuua,” Bw Odinga akasema jana alipokuwa akiendesha kampeni yake katika kaunti ya Pokot Magharibi.

Naibu Rais Dkt Ruto alimwomba msamaha Bw Odinga kufuatia tukio hilo akiahidi kwamba, chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kitawaadhibu wanachama

wake ambao huenda walihusika katika shambulio hilo.

Viongozi wa kisiasa, kidini na mashirika ya kijamii walilaani ghasia hizo wakisema zinaharibu sifa za nchi msimu huu wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua waliongoza wanasiasa kulaani tukio hilo huku Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i akionya wanasiasa dhidi ya kupanga ghasia.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM) Hassan Ole Naado jana alisema taharuki inaendelea kutanda kati ya mirengo miwili mikuu ya kisiasa nchini, na akaomba vyombo vya usalama viwe ange ili taifa lisielekee mkondo wa uchaguzi tata wa 2007.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA: Kibarua kizito kwa vikosi vya Afrika nchini...

Usahihishaji wa KCSE kuanza Jumatatu, atangaza Magoha

T L