• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
KRU yasema vikosi viko tayari kwa Ligi Kuu ya Kenya Cup

KRU yasema vikosi viko tayari kwa Ligi Kuu ya Kenya Cup

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) litaanza kutoa msaada wa fedha kwa vikosi vya Ligi Kuu ya Kenya wiki hii kwa nia ya kuwezesha wachezaji kufanyiwa vipimo vya corona kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kampeni za msimu huu kupulizwa mwishoni mwa Februari.

Mwenyekiti wa KRU, Oduor Gangla, amesema fedha hizo zitalenga kuondolea washiriki wa Kenya Cup mzigo mkubwa baada ya hazina zao kuathiriwa na janga la corona ambalo limevuruga kalenda ya michezo mbalimbali duniani.

“Msaada huo wa kifedha utaanza kutolewa kwa vikosi wiki hii ili kufanikisha shughuli ya wanaraga wa Ligi Kuu kufanyiwa vipimo vya Covid-19,” akasema kinara huyo katika mahojiano yake na Taifa Leo.

Kivumbi cha Kenya Cup kimepangiwa kuanza Februari 27 baada ya kurejelewa kwa raga kuidhinishwa na Wizara ya Michezo.

Kuanza kwa ligi hiyo kutatanguliwa na mchujo wa kubaini vikosi vitakavyopanda ngazi kushiriki Ligi Kuu ya Kenya Cup kutoka klabu za daraja la chini (Championship).

Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi itawaalika Wasps wa Chuo Kikuu cha Egerton wikendi hii ambapo mshindi atafuzu kuvaana na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro kwenye nusu-fainali ya Februari 13.

USIU-A watakutana na Northern Suburbs na mshindi atajikatia tiketi ya kumenyana na Strathmore Leos kwenye nusu-fainali nyingine.

Washindi wa nusu-fainali hizo mbili watajaza nafasi za Western Bulls na Kisumu RFC walioshushwa ngazi kwenye Kenya Cup mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Mechi za ligi zitakuwa za mkondo mmoja pekee msimu huu na zitachezwa kwa kipindi cha wiki 11 ambapo vikosi vinne vya kwanza vitafuzu kwa nusu-fainali ambazo zimeratibiwa kupigwa Mei 22 kabla ya fainali kufuata wiki moja baadaye.

Katika siku ya kwanza ya kampeni za Kenya Cup msimu huu, Impala watavaana na Kenya Harlequins, Homeboyz wapepetana na Nondies nao Mwamba washuke ugani kukwaruzana na Blak Blad. Oilers watakuwa wenyeji wa Nakuru RFC.

Gangla amesema pia KRU itafichua kocha mpya atakayedhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 wiki hii kabla ya kuanza shughuli ya kuteua kikosi kitakachowakilisha Kenya kwenye Raga ya Afrika kwa chipukizi almaarufu Barthes Cup.

Kenya ambayo imetiwa kwenye zizi moja na Zambia, Tunisia na Bukini, itakuwa mwenyeji wa kipute hicho 20 kuanzia Machi 25 hadi Aprili 4 jijini Nairobi.

Mshindi wa kivumbi hicho atafuzu kwa mapambano ya kuwania taji la dunia kwa chipukizi almaarufu Junior Rugby World Trophy kuanzia Septemba katika taifa litakalofichuliwa na Shirikisho la Raga la Dunia (WA) mwishoni mwa mwezi huu.

Chini ya mkufunzi Paul Odera, wanaraga chipukizi wa Kenya almaarufu Chipu, walitawazwa mabingwa wa kivumbi cha Barthes Cup mnamo 2019 baada ya kuwapokeza Namibia kichapo cha 21-18 kwenye fainali iliyoandaliwa jijini Nairobi.

Ushindi huo wa Chipu uliwakatia tiketi ya kunogesha Junior Rugby World Trophy nchini Brazil na wakaambulia nafasi ya tano mwishowe. Walipepeta wenyeji Brazil 26-24, wakapokezwa na Uruguay kichapo cha 63-11 na kucharazwa na 48-34 na Japan walioibuka kileleni mwa kundi.

Odera kwa sasa anadhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande, Kenya Simbas na nafasi aliyoicha kambini mwa Chipu inatazamiwa kutwaliwa na mkufunzi Paul Murunga.

Kati ya wachezaji waliopeperusha bendera ya Kenya kwenye kampeni za Barthes Cup miaka miwili iliyopita, ni wanaraga wanne pekee ambao wana uwezo wa kuwania nafasi ya kuwakilisha taifa kwa mara nyingine katika makala ya mwaka huu. Hao ni Mureithi Mwiti, Owain Ashley, Lorence Ishuga na George Kiriazi.

Ili kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Barthes Cup, KRU imethibitisha kuajiri wakufunzi wawili raia wa Afrika Kusini – Neil De Kock ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu ‘Springbok’ na Ernst Joubert ambaye ni nahodha wa zamani wa kikosi cha Saracens ili kupiga jeki juhudi za atakayekuwa kocha mpya wa Chipu.

You can share this post!

Gor Mahia kusajili wanasoka wawili zaidi wa kigeni

Wakenya njaa viongozi wakipiga domo