• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Kuwazia unachofanya na kukipenda ndio njia ya Kufaulu, Refa Lucy

Kuwazia unachofanya na kukipenda ndio njia ya Kufaulu, Refa Lucy

Na PATRICK KILAVUKA

Kuwa na matumaini katika ulitakalo huwa chimbuko la mawazo ya kujiwazia mema na kufaulu licha ya changamoto kuwepo kwa maisha ya mwanadamu!

Hiyo ni kauli ya refa Lucy Wanjiru, 24 ambaye anasema ingawa safari yake ya kuwa refa hakuwa rahisi. Refa huyu ambaye ni mzaliwa wa Njoro, Kaunti ya Nakuru na kupata masomo ya Msingi Shule ya Ngongogeri kabla kujiunga na Sekondari ya Ogilgei anasema ilianza kama mchezaji.

Refa Wanjiru alichezea kama difenda akiwa shule ya msingi hadi akapiga soka hadi kiwango cha Kaunti ya Nakuru na akiwa shule ya upili alikumbatia kabumbu hadi Kiwango cha Kanda ya Kusini mwa Bonde la Ufa.Ni baada ya kumaliza masomo ya upili, alipata fursa ya kujitanua katika fani ya soka kwa kujiunga na timu ya Kibagare Girls mwaka 2017 na kujituma 2019 na wakatwaa taji la Tim Wanyonyi Super kwa kushinda Kangemi Ladies 2-0 ugani CAVS.

Baada ya msambao wa corona kuyeyuka kiasi na milango ya soka kufunguliwa, muamuzi huyu alianza kusakamwa na kiu ya kuendeleza taaluma yake katika ulingo wa Kandanda na kuona kwamba njia ya pekee anaweza kufuatilia ndoto yake ni kuwa mpuliza kipenga mbali na kufanya kazi ya kutunza

usafi wa majumba kupitia kampuni ya Arrow Facilities. Alishawishiwa na kinara wa marefa tawi la Nairobi Magharibi Aggrey Shavera kupata fursa ya kujifunza kozi ya urefa kwa wiki moja na kupita mtihani wa kiwango cha gredi ya tatu. Baada ya mafunzo, alianza kuchezesha mechi za Shirikisho la Kandanda kaunti ndogo, Kaunti na Kanda mwaka jana.

Refa Lucy Wanjiru kati mwa uwanja kuchezesha mchuano katika White Eagles (jezi nyekundu) dhidi ya Kabete Pirates uwanjani Approved, Lower Kabete…Picha/PATRICK KILAVUKA

Mechi ya kwanza kuchezesha ilikuwa Uthiru Vision dhidi ya Kangemi PAG kama refa msaidizi kabla kuaminiwa uchezeshaji wa kati. Amechezesha mwaka huu kinganganyiro cha Westlands Youth Soccer Tournment almaarufu kama Tim Wanyonyi Super Cup kitengo cha shule za upili.

Alichezesha kwa busara kubwa pia mchuano wa Ligi ya Kaunti ndogo ya Kabete baina ya White Eagles dhidi ya Kabete Pirates na kuridhisha mashabiki na wadau wa timu hizo pasi na kuteleza katika wajibu wake urefa hu. Ari ya kufikia upeo wa taaluma yake ya urefa, imetokana na refa ambaye ni kielelezo chake refa wa Fifa Bruce Philiph na mwenyekiti wa marefa Shavera.

“Mawaidha ya wazoefu hao niliowataja kama kivutio changu, yamenifanikisha katika uwanja huu kwani yamenipanua kimawazo na kimaamuzi na wananihimiza kuzingatia kanuni za soka kujipiga jeki katika utekelezaji wa majukumu ya mpuliza firimbi,” anasema refa Lucy ambaye amebarikiwa mtoto Blessing Wairimu.

Yeye hujinoa kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa baada ya kazi kabla kuwajibishwa wikendi. Anasema kujihakikishia kwamba anakita mizizi, hujijasirika akiwa ugani, kuwa radhi kuendelea kusoma sheria za kandanda, kufanya mazoezi kwa bidii na kujinyanyua zaidi.

Changamoto ambaye amekumbana nazo ni mizomeo ya mashabiki ambao wanataka timu zao zishinde pasi na suala la kitaasubi. Anajipiga moyo konde kuwa refa wa Fifa usoni. Ushauri wake ni kwamba ukitakuwa refa,fuata ndoto yako na penda ikifanyacho

Refa Lucy Wanjiru akiwa na refa Amadi wakienda mapumziko baada ya mechi kipindi cha kwanza…Picha/PATRICK KILAVUKA

You can share this post!

Katibu mkuu kushtakiwa kwa kuchapa mke

TUSIJE TUKASAHAU: Umaskini na ukosefu wa intaneti...

T L