• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
KWPL: Kinyang’anyiro cha kiatu cha dhahabu chapamba moto

KWPL: Kinyang’anyiro cha kiatu cha dhahabu chapamba moto

NA AREGE RUTH

ZIMESALIA mechi tano Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) kufikia kikomo na vita vya kuwania kiatu cha dhahabu vinaendelea kupamba moto.

Washambulizi watano wakiwemo Monicah Etot wa Kisumu All Starlets na mabao (13) sawa na Wendy Atieno wa Thika Queens wanaongoza katika ufungaji mabao kutokana na mechi 17 za ligi.

Pure Alukwe wa Zetech Sparks (12), Jacline Chesang kutoka Wadadia Women (10) na Maureen Ater wa Vihiga Queens (10) wanafunga jedwali la wafungaji bora tano kwenye ligi.

Wakati uo huo, kocha wa makipa wa Gaspo Women James Ombeng anasema klabu hiyo ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Katika mechi za awali sita, Gaspo wamepata ushindi mara tano na kupiga sare moja.

Wanaongoza kwenye msimamo wa ligi na alama 40 sawa na Vihiga Queens lakini wanatofautiana na mabao sita.

Gaspo chini ya kocha mgeni Jacob ‘Ghost’ Mulee ambaye wakati mwingi hajumuiki na benchi la ufundi wakati wa mechi huwa anampa majukumu Ombeng kuongoza timu hiyo.

Akizungumza baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Bunyore Starlets Jumapili, Aprili 30, 2023 ugani Gems Cambridge, alisema ligi kwa sasa ina ushindani mkali.

“Kilichosalia sasa ni kushinda mechi zetu zote. Kikosi kiko sawa wachezaji wanajituma na hilo ndilo jambo la muhimu. Ushindani unaeendelea kuwa mgumu ikizingatiwa kwamba, wapinzani wetu Vihiga wako nasi bega kwa bega,” alisema Ombeng’.

Kwa upande wa kocha mkuu wa Bunyore Abisalom Mariga amesisitiza kuwa kupoteza mechi hiyo kulichangiwa na makosa ya wachezaji binafsi.

Bunyore walishuka hadi nafasi ya nane na alama 19 sawa na Zetech Sparks ambao wako nafasi ya saba.

Baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Nakuru City Queens Jumapili iliyopita ugani RVTI mjini Nakuru, Ulinzi walisalia nafasi ya tatu na alama 32 sawa Wadadia Women.

Mabingwa watetezi Thika Queens wanaendelea kuyumba yumba ligini. Wanafunga sita bora na alama 27, Kisumu All Starlets na Zetech Sparks wanashikilia nafasi ya nane na tisa wakiwa na alama 17 na 16 mtawalia.

Trans Nzoia Falcons, Kangemi Ladies na Kayole Starlets wanachungulia kushuka daraja katika nafasi ya 10,11 na 12 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto apokea Sh400 bilioni kuinua Bottom Up

Karua: Alhamisi kuna maandamano

T L