• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Leicester na PSV waumiza nyasi bure katika mkondo wa kwanza wa Europa Conference League

Leicester na PSV waumiza nyasi bure katika mkondo wa kwanza wa Europa Conference League

Na MASHIRIKA

PSV Eindhoven kutoka Uholanzi walilazimishia Leicester City sare tasa katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya Europa Conference League uwanjani King Power mnamo Alhamisi usiku.

Ingawa walianza mechi kwa matao ya juu, Leicester walisuasua pakubwa na kupoteza nafasi nyingi za wazi kupitia Harvey Barnes na Kelechi Iheanacho.

Nusura PSV wapate bao kupitia Mario Gotze aliyemtatiza sana kipa Kasper Schmeichel katika kipindi cha pili. Vikosi hivyo vitarudiana kwa mkondo wa pili mnamo Aprili 14, 2022 uwanjani Philips, Uholanzi. Mshindi wa mechi hiyo atakutana ama na AS Roma au Bodo/Glimt katika hatua ya nusu-fainali.

Leicester wananogesha soka ya bara Ulaya kwa mara ya pili katika historia baada ya kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) miaka mitano iliyopita baada ya kuibuka wafalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2015-16.

Walibanduliwa na Atletico Madrid ya Uhispania katika hatua ya 16-bora ya UEFA wakati huo wakiwa chini ya kocha Claudio Ranieri.

Kinyume na Leicester, PSV wanajivunia tajriba pevu katika soka ya bara Ulaya na waliwahi kutwaa taji la European Cup mnamo 1988.

Chini ya kocha Roger Schmidt, PSV kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) huku alama nne pekee zikiwatenganisha na viongozi Ajax. Hii ni mara yao ya tatu kushiriki soka ya bara Ulaya msimu huu.

Walidenguliwa kwenye kivumbi cha UEFA kabla ya kushuka hadi hatua ya makundi ya Europa League walikoambulia nafasi ya tatu kisha wakateremshwa hadi Europa Conference League.

Nafuu zaidi kwa Leicester ni rekodi duni ya PSV ambao wamepoteza mechi tisa kati ya 10 zilizopita kwenye robo-fainali za soka ya bara Ulaya.

MATOKEO YA EUROPA CONFERENCE LEAGUE (Alhamisi):

Feyenoord 3-3 Slavia Prague

Bodo/Glimt 2-1 AS Roma

Leicester City 0-0 PSV

Marseille 2-1 PAOK Salonika

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mtego wa Raila katika Azimio

Lewandowski abeba Bayern Munich dhidi ya Augsburg katika...

T L