• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Limbukeni Monza waangusha miamba Juventus katika Ligi Kuu ya Italia

Limbukeni Monza waangusha miamba Juventus katika Ligi Kuu ya Italia

Na MASHIRIKA

LIMBUKENI Monza waliduwaza miamba Juventus kwa kuwapokeza kichapo cha 1-0 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Jumapili.

Ushindi huo wa kihistoria ambao ulikuwa wa kwanza kwa Monza katika Serie A, ulizidisha masaibu ya kocha Massimiliano Allegri kambini mwa Juventus ambao sasa wanashikilia nafasi ya nane jedwalini kwa alama 10 sawa na Torino.

Juventus walikamilisha mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya fowadi Angel di Maria kuonyeshwa kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza. Hiyo ilikuwa mara ya 10 kwa nyota huyo raia wa Argentina kuonyeshwa kadi nyekundu katika taaluma yake ya usogora.

Monza inayomilikiwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Italia, Silvio Berlusconi, ilipandishwa ngazi kunogesha soka ya Serie A kwa mara ya kwanza mwishoni mwa msimu wa 2021-22.

Ushindi wao dhidi ya Juventus uliwaondoa mkiani mwa jedwali na kuwapaisha hadi nafasi ya 18 kwa alama nne, mbili zaidi kuliko Cremonese na Sampdoria.

Nyota wa timu ya taifa ya Italia – Matteo Pessina na Stefano Sensi pamoja na beki Pablo Mari anayeakata soka kwa mkopo kutoka Arsenal, ni miongoni mwa masogora wanaochezea Monza.

Juventus wameshinda mechi mbili pekee kutokana na saba zilizopita katika Serie A msimu huu. Aidha, wamepoteza michuano yote miwili ya ufunguzi wa kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu – PSG waliwatandika 2-1 mnamo Septemba 6, 2022 kabla ya Benfica kuwapokeza kichapo sawa na hicho mnamo Septemba 14, 2022.

MATOKEO YA SERIE A (Jumapili):

Monza 1-0 Juventus

AC Milan 1-2 Napoli

Udinese 3-1 Inter Milan

Cremonese 0-4 Lazio

Fiorentina 2-0 Hellas Verona

Roma 0-1 Atalanta

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Real wakung’uta Atletico kwenye gozi la La Liga

Amri ya Ruto ingali ni maneno matupu

T L