• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:42 PM
Liverpool guu moja ndani ya robo-fainali za UEFA baada ya kuzamisha Inter Milan

Liverpool guu moja ndani ya robo-fainali za UEFA baada ya kuzamisha Inter Milan

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL waliweka hai matumaini ya kuingia robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Inter Milan ya Italia mnamo Jumatano usiku ugani San Siro.

Dalili zote ziliashiria kwamba mechi hiyo ingekamilika kwa sare tasa hadi dakika ya 75 ambapo fowadi Roberto Firmino alijaza kimiani krosi ya Andrew Robertson. Mohamed Salah alipachika wavuni bao la pili la Liverpool katika dakika ya 83 na kuwaweka waajiri wake katika nafasi nzuri zaidi ya kusonga mbele wanaposubiri mkondo wa marudiano mnamo Machi 8, 2022 ugani Anfield.

Inter ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) walimiliki asilimia kubwa ya mpira na nusura wajiweke kifua mbele kupitia kwa Hakan Calhanoglu aliyeshuhudia kombora lake likibusu mwamba wa goli. Mabao ya Liverpool yalitokana na majaribio mawili na ya pekee katika lango la wenyeji wao.

Kiungo chipukizi Harvey Elliot aliweka historia ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa na Liverpool katika soka ya UEFA akiwa na umri wa miaka 18 na siku 318. Pigo la pekee kwa Liverpool ya kocha Jurgen Klopp katika mechi hiyo ni jeraha la kifundo cha mguu ambalo sasa linatarajiwa kumweka nje fowadi raia wa Ureno, Diogo Jota ambaye nafasi yake ilitwaliwa na Firmino mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Liverpool ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 54, sasa wameshinda mechi saba mfululizo katika mashidano yote yaliyopita. Inter walianza mchezo kwa matao ya juu na wakapoteza nafasi nyingi za kufunga mabao kupitia kwa Edin Dzeko, Ivan Perisic na Lautaro Martinez.

Liverpool wanafukuzia jumla ya mataji manne msimu huu na huenda watakuwa tayari wametia kapuni ubingwa wa Carabao Cup kufikia wakati watakaporudiana na Inter jijini Merseyside. Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool wamepangiwa kuvaana na Chelsea kwenye fainali ya Carabao Cup mnamo Februari 27, 2022 ugani Wembley, Uingereza.

You can share this post!

Bayern na Salzburg nguvu sawa katika mkondo wa kwanza wa...

Okiya Omtata ashtaki mahakama ya juu EACJ

T L