• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Liverpool mabingwa wa Carabao Cup

Liverpool mabingwa wa Carabao Cup

Na MASHIRIKA

KIPA Kepa Arrizabalaga aliyeletwa na Chelsea uwanjani mwishoni mwa muda wa ziada kuokoa penalti alipaisha mkwaju wake na kuwapa Liverpool ushindi wa 11-10 baada ya sare tasa chini ya dakika 120.

Ufanisi huo unaweka hai matumaini ya Liverpool kukamilisha kampeni za msimu huu wakijivunia jumla ya mataji manne kwa mara ya kwanza katika historia. Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool pia wanafukuzia mataji ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mlinda-lango wa Liverpool, Caoimhin Kelleher, 23, aliaminiwa na Klopp kuchukua nafasi ya kigogo Alisson Becker katikati ya michuma. Alifungia waajiri wake penalti ya 11 kabla ya Kepa aliyejaza nafasi ya Edouard Mendy kutokana na umahiri wake wa kupangua penalti, kuyeyusha ndoto za Chelsea za kunyanyua taji la Carabao Cup kwa mara ya sita.

Liverpool sasa wameweka rekodi ya kutwaa kombe la Carabao Cup ambalo huandamana na tuzo ya Sh15 milioni mara tisa katika historia. Fainali ya Jumapili usiku ilikuwa yao ya kwanza kunogesha katika kipute hicho tangu 2012.

Arsenal na Tottenham Hotspur walioaga kivumbi hicho katika hatua ya nusu-fainali walitia kapuni Sh3.75 milioni kila mmoja huku Chelsea wakiridhika na Sh7.5 milioni.

Ingawa Liverpool walijiundia nafasi nyingi za kufunga na kushuhudia bao la Joel Matip katika kipindi cha pili likikataliwa, Chelsea walipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Mason Mount, Christian Pulisic, Romelu Lukaku, Kai Havertz na Timo Werner huku mabao yao matatu yakifutiliwa mbali.

Kepa ambaye ni raia wa Uhispania aliwahi kukataa kuondoka uwanjani mnamo 2019 aliyekuwa kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri, alipokifanyia kikosi chake mabadiliko dhidi ya Manchester City kwenye fainali ya Carabao Cup.

Baadaye Agosti 2021, aliongoza waajiri wake kuzoa taji la Uefa Super Cup baada ya Chelsea kupepeta Villarreal ya Uhispania kwa penalti 6-5 jijini Belfast, Northern Ireland.

Mbali na Caoimhin, masogora wengine walioridhisha zaidi kwa upande wa Liverpool ni sajili mpya Luis Diaz na Sadio Mane aliyemtia Mendy kwenye mizani katika kipindi cha kwanza.

Liverpool wataalika Norwich City kesho kwa mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA kabla ya kupepetana na West Ham United katika EPL ugani Anfield na kuwa wenyeji wa Inter Milan kwenye marudiano ya hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Machi 8, 2022. Baadaye watavaana na Brighton, Arsenal na Manchester United kwa usanjari huo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

ReplyForward
  • Tags

You can share this post!

Marefarii Thika kupewa mafunzo

Aubameyang aongoza Barcelona kuzamisha Bilbao katika La Liga

T L