• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Liverpool, Manchester City nguvu sawa ligini

Liverpool, Manchester City nguvu sawa ligini

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City pamoja na Liverpool walitarajia kudengua Chelsea kudengua Chelsea kileleni mwa jedwali waliposhuka dimbani kupimana ubabe uwanjani Anfield mnamo Jumapili.

Hata hivyo, sare iliyosajiliwa na vikosi hivyo ilidumisha masogora wa kocha Thomas Tuchel kileleni mwa jedwali la EPL.

Man-City walitamalaki kipindi cha kwanza cha mchezo ila wakapoteza nafasi nyingi za wazi. Waliadhibiwa baadaye na Sadio Mane aliyeshirikiana vilivyo na Mohamed Salah katika dakika ya 59.

Hata hivyo, uongozi wa Liverpool ulidumu kwa dakika 10 pekee kabla ya Phil Foden kumzidi ujanja James Milner na kukamilisha krosi ya Gabriel Jesus.

Salah alifungia Liverpool bao la pili katika dakika ya 76 kabla ya kombora lililovurumishwa na Kevin De Bruyne katika dakika ya 81 kumbabatiza beki Joel Matip na kujaa ndani ya lango lililokuwa chini ya ulinzi wa Alisson Becker.

Kufikia sasa, Liverpool ya kocha Jurgen Klopp inajivunia alama 15, moja pekee kuliko Chelsea ambao wamepoteza mechi moja na kuambulia sare mara moja kutokana na michuano saba iliyopita ya EPL msimu huu.

Man-City kwa upande wao wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 14 sawa na Manchester United, Everton na Brighton.

Ushindi kwa Man-City ungeshuhudia Liverpool wakipoteza mechi yao ya kwanza ligini muhula huu. Mabingwa hao wa EPL 2019-20 ndicho kikosi cha pekee ambacho hakijapigwa ligini hadi kufikia sasa muhula huu.

Man-City walishuka dimbani wakipania kujinyanyua baada ya Paris Saint-Germain (PSG) kuwalaza 2-0 katika mechi iliyopita ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Liverpool nao walikuwa wakilenga kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya FC Porto ya Ureno kwenye kipute hicho cha bara Ulaya ugani Estadio do Dragao.

Japo matokeo ya Liverpool katika UEFA yamekuwa yakiridhisha baada ya kufungua kampeni zao kwa ushindi wa 3-2 ugani Anfield, uthabiti wao ligini ulitikiswa na limbukeni Brentford waliowalazimishia sare ya 3-3 katika mchuano uliotangulia kabla ya kumenyana na Man-City.

Liverpool sasa hawajapoteza mechi katika jumla ya mapambano 11 yaliyopita ugani Anfield na wamefunga mabao 17 kutokana na mechi saba zilizopita ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

FAO yahimiza vijana wawe mstari wa mbele katika shughuli za...

Mshindi wa zamani wa taji la Ballon d’Or, Hegerberg,...