• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Liverpool walipua Man-City katika gozi la Community Shield

Liverpool walipua Man-City katika gozi la Community Shield

Na MASHIRIKA

WASHIKILIZI wa Kombe la FA, Liverpool, walituma onyo kali kwa wapinzani wao wakuu msimu huu baada ya kukomoa Manchester City ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) 3-1 katika pambano la Community Shield mnamo Jumamosi usiku.

Ni mechi iliyowapa Darwin Nunez wa Liverpool na Erling Haaland wa Man-City jukwaa mwafaka la kudhihirisha ubabe wao uwanjani. Wavamizi hao wawili ni miongoni mwa sajili wapya wa EPL watakaolekezewa na mashabiki macho ya karibu zaidi muhula huu wa 2022-23.

Nunez alitokea benchi katika kipindi cha pili na kufungia Liverpool bao la tatu, dakika chache baada ya kuchangia penalti iliyojazwa kimiani na Mohamed Salah. Awali, alikuwa amepachika wavuni magoli manne katika ushindi wa 5-0 uliosajiliwa na Liverpool dhidi ya RB Leipzig kirafiki uwanjani Red Bull Arena, Ujerumani mnamo Julai 21, 2022.

Bao jingine la Liverpool dhidi ya Man-City mnamo Jumamosi lilijazwa kimiani na beki Trent Alexander-Arnold huku masogora wa mkufunzi Pep Guardiola wakifutiwa machozi na sajili mpya, Julian Alvarez, aliyetokea River Plate ya Argentina kwa Sh2 bilioni.

Huku Nunez akitamba ndani ya jezi ya Liverpool, Haaland aliyeshawishiwa na Man-City kubanduka Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa Sh7.5 bilioni, alipoteza nafasi nyingi za wazi huku akiwa sasa na presha ya kujaza kwa kikamilifu mapengo yaliyoachwa na Raheem Sterling na Gabriel Jesus waliotua Chelsea na Arsenal mtawalia.

Nunez, 23, alisajiliwa na Liverpool kutoka Benfica ya Ureno kwa Sh12.6 bilioni baada ya kupachika wavuni mabao 34 kutokana na michuano 41 mnamo 2021-22. Magoli 26 kati ya hayo yalitokana na mechi 28 za Ligi Kuu ya Ureno.

Kutua kwake ugani Anfield kulichochewa na haja ya kujaza pengo la fowadi matata raia wa Senegal, Sadio Mane, aliyeyoyomea Bayern Munich ya Ujerumani. Nunez anatarajiwa kushirikiana zaidi na Salah na Roberto Firmino katika safu ya mbele ya Liverpool ambayo pia inajivunia huduma za Luis Diaz na Diogo Jota.

“Tutarajie makuu zaidi kutoka kwa wanasoka hawa ambao wana kiu ya kushinda kila kitu. Ni mwanzo wa msimu na kazi imeanza rasmi. Tuko imara na uthabiti huo unatuweka katika nafasi nzuri ya kupigania makombe yote Uingereza, Ulaya na duniani,” akasema kocha Jurgen Klopp wa Liverpool.

Liverpool walinyanyua FA Cup na Carabao Cup mnamo 2021-22 na waliweka hai matumaini ya kuweka historia ya kuzoa mataji manne katika kampeni za msimu mmoja hadi wiki ya mwisho ambapo walipigwa kumbo na Man-City kwenye EPL na Real Madrid kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Guardiola anaamini kuwa Haaland aliyefunga mabao 86 kutokana na mechi 89 kambini mwa Dortmund, atajinyanyua hivi kadri Man-City wanavyolenga kutwaa taji la UEFA kwa mara ya kwanza na kufikia pia rekodi ya Man-United waliowahi kujizolea ufalme wa EPL mara tatu mfululizo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ndondi: Okoth ajikwaa mashindano ya Madola nchini Uingereza

TAHARIRI: Kuficha unga wa mahindi ni hujuma

T L