• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
TAHARIRI: Kuficha unga wa mahindi ni hujuma

TAHARIRI: Kuficha unga wa mahindi ni hujuma

NA MHARIRI

UFICHUZI wa Waziri wa Kilimo Peter Munya kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanaficha unga wa mahindi wa bei nafuu huku Wakenya wakiendelea kuteseka kutokana na hali ngumu ya maisha unaonyesha kiwango cha juu cha tamaa, kutojali na kutowajibika.

Akiwa kwenye mkutano wa kisiasa kaunti ya Nandi, Waziri Munya alisema kwamba serikali inafanya uchunguzi kubaini wanaoficha unga wa mahindi hata baada ya serikali kutoa afueni kwa mahindi yanayoingizwa nchini ili kupunguza gharama ya uzalishaji kwa manufaa ya Wakenya masikini.

Alisema kwamba watakaopatikana wamehusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Inasikitisha kwamba wafanyabiashara wamejawa na tamaa na ukatili wa kuweza kuficha bidhaa ambayo serikali imechukua hatua kupunguzia bei raia wake mzigo.

Inasitikisha Bw Munya alifichua hayo katika mkutano wa kampeni za kisiasa licha ya kuwa Wakenya wamekuwa wakililalamika kwa muda zaidi ya wiki mbili kuwa unga huo wa bei nafuu haupo madukani. Hata hivyo, la muhimu hapa sio tangazo na lilikotolewa, ni iwapo uchunguzi huo utazaa matunda.

Ikizingatiwa hali ambayo Wakenya wanapitia wakati ambao kiwango cha mfumuko wa gharama ya maisha kimefikia asilimia 8.3 mwishoni mwa mwezi jana, kuna haja ya serikali kuchukua hatua, sio kwa maneno, mbali kwa vitendo kwa kuwa wafanyabiashara hao wanataka kunufaika na pesa za mlipa ushuru huku mlipaji ushuru huo akiendelea kuteseka.

Watu kama hao na washirika wao wakiwemo walio serikalini wanafaa kupokonywa leseni zao na kushtakiwa kwa kuhujumu usalama na uchumi wa nchi.

Watu kama hao na washirika wao wanafaa kupigwa marufuku kushiriki biashara ya bidhaa za chakula nchini kwa sababu kuficha unga wa mahindi katika nchi ambayo raia wake wengi huutumia kwa chakula ni sawa na kujaribu kuua halaiki.

Hii ni hatua ambayo serikali ingechukua chini ya maji na matokeo kuonekana wazi kwa kuwa lengo kuu la serikali ni kulinda raia wake na mali yao.

Hii inamaanisha kuwa uchunguzi huo unafaa kufanywa ndani ya idara husika za serikali kubaini maafisa wanaoshirikiana na wafanyabiashara hao. Serikali ina uwezo wa kufanya hivyo na kuokoa Wakenya.

Serikali inafaa kulinda raia wake kila wakati na sio kusubiri walillamika ili iweze kuchukua hatua.

You can share this post!

Liverpool walipua Man-City katika gozi la Community Shield

Mgombeaji wa ugavana Kilifi ajiondoa na kuunga mkono Kithi

T L