• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Liverpool wapewa Man-City, Palace wakivaana na Chelsea nusu-fainali za Kombe la FA

Liverpool wapewa Man-City, Palace wakivaana na Chelsea nusu-fainali za Kombe la FA

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL watakuwa na kibarua kigumu cha kusonga mbele katika Kombe la FA msimu huu baada ya kukutanishwa na mabingwa mara sita Manchester City katika nusu-fainali ya Aprili 16.

Crystal Palace walioponda Everton 4-0 katika hatua ya nane-bora, watamenyana na Chelsea mnamo Aprili 17. Mechi zote za nusu-fainali zitasakatiwa ugani Wembley, Uingereza. Chelsea walitinga fainali ya Kombe la FA msimu jana na wakakomolewa na Leicester City kwa bao 1-0. Palace hawajawahi kunyanyua Kombe la FA katika historia yao.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walitawazwa wafalme wa Kombe la FA mara ya mwisho mnamo 2019 baada ya kuponda Watford 6-0. Liverpool kwa upande wao wametwaa ubingwa wa taji hilo mara saba, mara ya mwisho ikiwa 2006 baada ya kuzamisha West Ham United kwa penalti 3-1 jijini Cardiff.

Liverpool wanaopigania jumla ya mataji manne msimu huu, walifuzu kwa nusu-fainali za kipute hicho baada ya kupokeza Nottingham Forest kichapo cha 1-0 mnamo Jumapili. Bao hilo la pekee lilijazwa kimiani na fowadi matata raia wa Ureno, Diogo Jota.

Chelsea walitandika Middlesbrough 2-0 katika robo-fainali ugani Riverside mnamo Jumamosi kabla ya Man-City kucharaza Southampton 4-1 uwanjani St Mary’s siku moja baadaye.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool watalazimika kuzamisha Man-City ili kuweka hai matumaini ya kuandikisha historia ya kuwa kikosi cha kwanza katika soka ya Uingereza kuwahi kunyanyua jumla ya mataji manne katika muhula mmoja.

Baada ya kukomoa Chelsea kwa penalti 11-10 na kunyanyua Carabao Cup wiki tatu zilizopita, Liverpool sasa wanafukuzia mataji matatu zaidi msimu huu – Kombe la FA, Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kufikia sasa, wametinga robo-fainali ya UEFA itakayowakutanisha na Benfica ya Ureno na wanashikilia nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL kwa alama 69, moja pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Man-City.

Japo Liverpool wana motisha ya kuweka historia, kibarua dhidi ya Man-City hakitakuwa chepesi ikizingatiwa ugumu wa ratiba yao kabla ya kukutana na wapambe hao ambao ni washindani wao wakuu ligini.

“Tutakutana na Watford, Benfica, Man-City, Benfica, Man-City, Man-United kisha Everton kwa usanjari huo baada ya likizo fupi itakayopisha michuano ya kimataifa. Hizi ni mechi ngumu ambazo tutalazimika kutandaza moja baada ya nyingine,” akasema mkufunzi wa Liverpool, Jurgen Klopp.

“Tulifahamu hata kabla ya kuvaana na Nottingham kwamba tungekutana na Man-City kwenye nusu-fainali za Kombe la FA. Sasa tumeyavulia maji nguo na hatuna budi kuoga. Hakuna kikosi ambacho hutamani kukutana na Liverpool. Man-City pia wanatuogopa na tuko tayari kuwatoa kijasho,” akaongeza Klopp.

DROO YA 4-BORA FA CUP:

Chelsea vs Crystal Palace

Man-City vs Liverpool

  • Tags

You can share this post!

Boga aomba ODM tiketi bila mchujo

Hatukudhamini utafiti wa Infotrak kwa nia mbaya, Haki...

T L